Habari za Kitaifa

Mwanahabari Rita Tinina aliaga dunia kutokana na nimonia – Upasuaji

March 19th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MWANAHABARI Rita Tinina aliaga dunia kutokana na matatizo ya kiafya yaliyosababishwa na ugonjwa wa nimonia ambao huathiri mapafu, matokeo ya upasuaji wa maiti yameonyesha.

Akiongea Jumanne katika hifadhi ya maiti ya Umash, msemaji wa familia Timothy Nyaga alisema wameridhishwa na matokeo hayo.

“Tulifika hapa kushuhudia upasuaji wa maiti na uliendeshwa na Dkt Peter Ndegwa na mwanapatholojia wa familia. Tumepewa matokeo kwamba Rita aliaga dunia kutokana na nimonia,” akasema Bw Nyaga.

Aidha Bw Nyaga alithibitisha kuwa upasuaji wa maiti hiyo ulifanywa huku mwanapatholojia wao akiwepo.

Aliongeza kuwa familia ingali inasisitiza haja ya kuruhusiwa kuomboleza kwa faragha wakati huu wa majonzi.

“Ikumbukwe kwamba kuna familia iliyopoteza mpendwa wao,” Bw Nyaga akasisitiza huku akishukuru wanahabari waliotoa rambirambi zao na kumtunuka sifa marehemu Tinina.

Tinina almaarufu RT, alipatikana akiwa ameaga dunia nyumbani kwake katika mtaa wa Kileleshwa, Nairobi mnamo Jumapili.

Alipatikana katika chumba chake cha kulala na mjakazi wake.