Michezo

Mwanahabari sasa alia amzalie Rooney

June 20th, 2020 2 min read

CHRIS ADUNGO

MWANAHABARI Helen Wood, aliyewahi kuchunwa ngozi na mvamizi wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Wayne Rooney kisha kumfichulia Coleen (mkewe Rooney) siri ya uhusiano wao wa kimapenzi sasa kamwamkia upya.

Helen ambaye alitawazwa mshindi wa Big Brother America mnamo 2014, anamtaka Rooney, 34, arudiane naye iwapo kwa kweli anataka mtoto wa kike.

Na katika ungamo lililolenga kuonyesha udhati wa anachokimaanisha, kichuna huyo mwenye umri wa miaka 33 ametishia kuandika na kuchapisha kitabu kitakachosimulia yote yaliyojiri kati yake na Rooney iwapo sogora huyo hatasalimu amri na kuanza kulidokoa upya tunda lake hadi apate ujauzito. Rooney kwa sasa ni nahodha na kocha msaidizi wa Derby County, Uingereza.

Helen ambaye ni mama wa mtoto mmoja, nusura aivunje ndoa ya Rooney na Coleen yapata miaka tisa iliyopita alipopasua mbarika kuhusu jinsi ambavyo mwanasoka huyo wa zamani wa Everton alivyokuwa akimshawishi mara kwa mara kwa kiasi kikubwa cha fedha ili kulitalii buyu lake la asali bila ya mkewe kujua.

Wakati Helen alipomwaga mtama huo penye kuku wengi, Coleen alikuwa na ujauzito wa miezi mitano katika safari ya kumtarajia mtoto wake wa pili, Kai Wayne.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Star, Helen ambaye amekiri aliwahi kuwa kahaba, tayari ameanza kushauriana na mashirika mbalimbali ya uchapishaji kwa lengo la kufyatua kitabu kitakachofunua siri nyingi za mahusiano yake ya kimapenzi na zaidi ya wanasoka 50 maarufu waliowahi kujirinia asali mzingani mwake kwa kitita kinono cha fedha.

Tishio la Helen linajiri miezi michache baada ya Coleen kuweka wazi ukubwa wa kiu yake ya kupata mtoto wa kike na Rooney ambaye alikuwa ameirudia mienendo yake ya zamani ya kutoka kimapenzi na makahaba wa kila sampuli kwenye maeneo ya burudani.

Tangu aanze kuhusiana na Rooney kimapenzi wakiwa na umri wa miaka 16 kisha kufunga pingu za maisha mnamo 2008, ndoa ya Coleen na mumewe imejaliwa watoto wanne wa kiume: Klay Anthony, Kai, Kit Joseph na Cass Mac.

Katika ziara yao ya mwisho kwenye ufuo wa Ibiza, Uhispania mnamo Januari 2020, Coleen aliandika na kupakia ujumbe huu kwenye Instagram kabla ya kuufuta saa chache baadaye:

“Kiu ya mtoto wa kike. Nina hamu sana. Hamu ambayo natumai itamaliziwa na Rooney hapa Ibiza kabla ya likizo hii fupi ya majuma machache kutamatika. Itakuwa furaha yangu kuangusha toto la kike mara hii.”