Habari Mseto

Mwanahabari wa K24 apatikana amefariki Molo

May 25th, 2020 1 min read

Na JOHN NJOROGE

MWILI wa mwanahabari wa shirika la K24 eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru, ulipatikana ukinging’inia kwa mti katika shamba la Gatura, Elburgon jana mchana.

Akithibitisha tukio hilo, naibu wa chifu, Bw Simon Kinuthia alisema mwili wa George Kori, 31 ulipatikana na umma ambao walikuwa wakitafuta aliko.

“Mwili wa marehemu ulipatikana kichakani ukining’inia kwa mojawapo ya miti katika shamba la wazazi wake,” Bw Kinuthia alisema, akiongeza kuwa familia yake ilipiga ripoti afisini kwake Alhamisi, Mei 21, siku mbili baada ya kutoweka kwake.

Katika mahojiano ya simu na Taifa Leo, Bw Kinuthia alisema alikusanya vijana wa eneo hilo na kuanza kumtafuta katika shamba lao.

Mamake, Bi Nancy Njeri, alisema marehemu alikuwa kifungua mimba wake katika familia ya watoto watano. Pia alimtaja kuwa mtiifu, mnyamavu na mwenye nidhamu na mwisho alionekana Jumanne jioni.

“Marehemu alikuwa na shinikizo la mawazo na kila mtu katika familia alijua hilo. Alikuwa bado anaendelea na matibabu ingawa alikuwa mwenye bidii sana,” shangazi yake, Bi Lucy Wanjiku alieleza.