Habari Mseto

Mwanahabari wa NMG kati ya walionusurika ajalini Sachang’wan

May 27th, 2024 1 min read

NA ERIC MATARA

ABIRIA mmoja alifariki na wengine 10 wakapata majeraha Jumapili asubuhi, baada ya matatu ya abiria 14 waliyokuwa wakisafiri nayo kwenye Barabara Kuu ya Nakuru-Eldoret kuhusika kwenye ajali ilipogonga trela katika eneo la Sachang’wan.

Kulingana na Kamanda wa Polisi Kaunti ya Nakuru, Bw Samuel Ndanyi, matatu hiyo, iliyokuwa ikisafirisha abiria kutoka Nairobi kuelekea Kisumu, ilikuwa ikijaribu kupita trela wakati wa ajali hiyo ya saa kumi na moja alfajiri.

“Matatu ilikuwa maeneo ya Jolly Farm, karibu na Sachang’wan, ilipogonga trela kutoka nyuma. Mtu mmoja alifariki papo hapo na wengine zaidi ya 10 wakapelekwa katika hospitali ndogo ya Molo kwa matibabu,” alisema Bw Ndanyi.

Hata hivyo, wengi wa abiria walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Mwanahabari wa Nation Media Group, Bw Charles Wasonga, ambaye alikuwa akisafiri kuelekea Kisumu, alikuwa miongoni mwa abiria waliojeruhiwa katika ajali hiyo.

“Nilipata majeraha madogo kwenye mguu wangu wa kushoto, lakini niliweza kupanda matatu nyingine hadi Kisumu. Nilifanyiwa uchunguzi na kutibiwa katika Hospitali ya Avenue jijini humo kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani,” aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu.