Habari Mseto

Mwanaharakati ajifunga mnyororo kwenye mnara wa Dedan Kimathi

September 14th, 2020 2 min read

NA CHARLES WASONGA

MWANAMUME mmoja alizua kioja katikati ya jiji la Nairobi Jumatatu, Septemba 14, alipojifunga kwa mnyororo katika sanamu ya Dedan Kimathi kama ishara ya kukerwa na ongezeko la visa vya wasichana kupachikwa mimba nchini.

Mnara huo uko katika makutano ya barabara za Kimathi na Mama Ngina, katikati mkabala na mkahawa wa Hilton.

Mwanaharakati huyo ambaye alivalia fulana nyeupe iliyoandikwa jina, “Chris wa under 18” alibeba bango lenye maandishi ya kuihimiza serikali kudhibiti visa vya wasichana chini ya umri wa miaka 18 kupachikwa mimba.

Maneno hayo yalisoma hivi: “Over 150K teenage pregnancies in a period of 4 months! Kenya is losing a generation by not addressing teenage pregnancies candidly!” “Zaidi ya wasichana 150,000 waliobaleghe wamepachikwa mimba ndani ya kipindi cha miezi minne! Kenya inapoteza kizazi kwa kutoshughulikia visa hivi vya mimba za mapema kwa ukakamavu!”

Mwanamume huyo alitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kutangaza mikakati ya kuzuia uovu huo ambao alisema utapelekea wasichana wengi kukosa kurejea shuleni baada ya janga la corona kudhibitishwa.

“Rais Kenyatta anafaa kushughulikia tatizo hili haraka iwezekanavyo. Nimejifunga hapa kwa sanamu ya Shujaa Dedan Kimathi katik juhudi za kuhakikisha kuwa ujumbe wangu unachukuliwa kwa uzito,” akasema jamaa huyo ambaye anajiita “mtetezi wa haki za wasichana walio chini ya umri wa miaka 18.”

Watu wengi walifika hapo kujionea kioja hicho. Maafisa wa polisi pia walikupewa wakijaribu kudhibiti msongamano wa magari. PICHA/ CHARLES WASONGA

Mnamo Julai, mwaka huu wa 2020 habari kuhusu visa vya wanafunzi wa kike kupachikwa mimba wakati huu wa janga la Covid-19 ziligongwa vichwa vya habari.

Kwa mfano, Idara ya Watoto katika Kaunti ya Machakos iliripoti kuwa karibu wasichana 4,000 ambao ni wanafunzi walipakwa mimba katika kaunti huu wakati wa “Lockdown” kudhibiti msambao wa virusi vya corona.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu na Watoto (UNICEF) pia zilionya kuhus ongezeko la visa vya watoto wa kike kudhulumiwa kimapenzi na kutungwa mimba haswa katika mataifa mengi barani Afrika. Asasi hizo zilisema baadhi ya wahusika katika vitendo hivyo ni watu wenye uhusiano wa kinasaba na waathiriwa.