Makala

Mwanaharakati aliye mstari wa mbele kuhakikisha mtoto wa kike anapiga hatua kimaisha

September 18th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

RUTH Juliet Ochieng, 19, ni mwanaharakati wa kike na mtetezi wa haki za kibinadamu kutoka Kibera katika Kaunti ya Nairobi.

Ruth ambaye anatoka katika familia ya kipato cha chini ameona wasichana wengi wakikabiliwa na changamoto nyingi.

Yeye anasema kwake imekuwa rahisi kwa sababu ana dada wakubwa ambao walielewa changamoto anazokabili mtoto wa kike wakati anakua katika maeneo ya Kibera.

Anatetea haki za wanawake na pia yuko mstari wa mbele kuhakikisha haki zingine za kibinadamu zinazingatiwa.

Yeye ndiye mkurugenzi mwenza wa Kituo cha Feminist for Peace Rights and Justice Centre (FPRJC) ambacho kinashughulikia maswala ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Katika kituo cha wanawake, tunaokoa na kuwakaribisha wahasiriwa wa Ukatili wa Kijinsia (GBV) kwa muda wa saa arobaini na nane na kisha kuwaunganisha na maeneo mengine ambako wanaweza kuokolewa kwa kipindi kirefu. Katika kituo hicho tunajitahidi kubadilisha waathiriwa kuwa manusura kwa kutoa msaada wa kisaikolojia na pia kupigania haki zao,” anasema.

Akifanya kazi kama mkurugenzi mwenza wa FPRJC, Ruth anawashauri wasichana waliobalehe na kuwawezesha katika masuala ya afya ya uzazi, mstakabali wa kijinsia na haki pamoja na ujuzi wa uongozi. Anakutana na wasichana kila wiki katika kituo hicho.

Wasichana hawajishughulishi tu na kujifunza lakini kuna siku zilizowekwa kwa shughuli za kujifurahisha na kubadilishana mipango kutoka kwa makazi tofauti.

Ruth ambaye kwa sasa anasomea shahada ya digrii ya Usalama na Masuala ya Sera alianza kutengeneza sabuni wakati karibu kila kitu kilisimama kipindi cha janga la Covid-19.

Kupitia msaada wa mashirika na marafiki kikundi kimeweza kuanzisha mradi na kuendelea nao vizuri.

“Sababu za kutengeneza sabuni ni kwa shughuli za usambazaji na mapato. Kama shughuli ya kuongeza mapato niliangalia uendelevu wa sabuni na nikaamua kuwa itafanya vizuri hata baada ya janga la Covid-19. Sabuni inauzwa kwa bei rahisi ambapo lita huenda kwa Sh60,” anasema.

Ruth anafanya kazi na timu ya watu kumi. Wamekuwa wakilenga kaya mia kwa mwezi lakini pia ni suala la kubadilika kwa hivyo kunapokuwa na shughuli wanapunguza bei ya sabuni yao.

Sabuni katika chupa. Picha/ Margaret Maina

“Ukweli ni kwamba watu wengine hawawezi kununua sabuni kwa hivyo wakipewa ina jukumu kubwa katika maisha ya mtu na inasaidia kuzuia virusi. Wakati wa kusambaza sabuni, sisi pia hupeana barakoa,” anaongeza.

Timu hiyo pia hufundisha watu kutengeneza sabuni. Katika kituo cha wanawake pia kuna maktaba ya jamii na sababu ya kutenga nafasi hiyo ni kujenga tabia ya mazoea ya kusoma miongoni mwa wanafunzi walioko Kibera.

Maktaba huchukua angalau wanafunzi 15 lakini kwa sababu ya janga maktaba haiwezi kuchukua mtu yeyote.

Milango ya maktaba ikiwa imefungwa, Ruth na timu yake wamekuwa na mkakati wa kufikiria tena kuhakikisha wanafunzi wa makazi duni wanaendelea kupata vifaa vya kujifunzia.

Hivyo, usambazaji wa vitabu na vitabu vya hadithi unafanya kazi vizuri. Wakati lengo kuu hapo awali lilikuwa katika kuwezesha mtoto wa kike, kwa sasa usambazaji wa vitabu sasa linawahusisha jinsia zote.

“Tunataka utamaduni wa kujifunza uendelee kati ya jamii yetu licha ya changamoto zilizoletwa na janga la Covid-19.

Hatuwezi kuzingatia kanuni ya watu kukaa kwa umbali wa zaidi ya mita mmoja baina yao katika maktaba yetu kwa sababu ni ndogo sana na ndiyo sababu tuliona umuhimu wa kusambaza vitabu vya maktaba yetu kwa nyumba zao,” anasema.

Wakati wa janga hili timu inahimiza jamii kukaa salama na kufuata hatua zilizowekwa na serikali.

Ruth na timu yake pia wanahimiza wanajamii wawe watu wa kuaminika katika ndoa zao na wale waliofika umri wa utu uzima na wako na wapenzi, wanawahimiza kudumisha kinga kuepuka magonjwa ya zinaa na mimba ambazo hawajapanga.