Kimataifa

Mwanajeshi aadhibiwa kwa kuajiri makahaba 10 jeshi likiwa kazini

January 14th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAJESHI wa kikosi cha Amerika wa kitengo cha Kapteni alivuliwa mamlaka na usimamizi wa jeshi la nchi hiyo, baada ya kuwaajiri mahawara kumi, wakati kikosi chake kilikuwa misheni Ufilipino.

Kapteni Travis Zettel baada ya kufanya hivyo alidaiwa kupoteza imani ya wakubwa wake, hivyo akavuliwa mamlaka kuongoza vamizi walipokuwa wakitumia meli ya USS Bremerton, baada ya uchunguzi kufanywa.

Idara ya kuchunguza visa vya kijinai ya jeshi la majini la US ilianzisha uchunguzi wake baada ya kudokezewa kuhusu kisa hicho.

Idara hiyo iliripotiwa kuwa Bw Zettel aliamrisha wasichana kumi kufika hotelini ambapo wanajeshi walikuwa wakiishi, kisha kamanda huyo akaonekana nao, wakiwa “wamevalia kihawara nje ya mlango wa mbele wa hoteli.”

Mtu mwingine aliyekuwa akisafiri kwa meli hiyo alisema kuwa Bw Zettel alionekana akiwa na “wasichana watatu wa eneo hilo wakimshikilia mkono walipokuwa wakizurura” na kuwasalimu wasafiri akiwa katika sehemu yake ya mamlaka.

Alipokumbwa na madai hayo na idara hiyo ya uchunguzi ya NCIS, kapteni huyo ailikiri madai kuwa aliwalipa wanawake hao kusafiri naye, nakala zikasema.

Kutokana na kisa hicho kilichofanyika Machi, mnamo Agosti, Bw Zettel aliadhibiwa kwa kuvuliwa mamlaka na kupelekwa katika kikosi kingine.

Hata hivyo, haikufahamika ni wasafiri wangapi ama wafanyakazi ambao walikuwa katika meli hiyo wakati kisa hicho kilipotendeka.