Michezo

Mwanamitindo wa kunyanyua vyuma afunguka ana mimba ya Vidal

June 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO wa Barcelona na timu ya taifa ya Chile, Arturo Vidal kwa sasa anatarajia kuwa baba baada ya mchumba wake Sonia Isaza kufichua kwamba amefungwa bao kabambe la kimapenzi na anajiandaa kuanza kuhudhuria kliniki.

Akishindwa kabisa kuyaficha matarajio yake hayo, Sonia ambaye ni mwanamitindo maarufu wa kunyanyua vyuma na vitu vya uzani mkubwa, alipakia kwenye mtandao wake wa Instagram picha zake za ujauzito na kuambatanisha maandishi: “Punde tutakuwa familia ya watatu”.

Isitoshe, kichuna huyo alifichua kwamba Vidal alimfunga bao hilo litakalohesabiwa rasmi mnamo Novemba 2020 walipokuwa wakiponda raha na kusherehekea siku ya wapendanao ya Valentino mnamo Februari 14 mwaka huu.

Sonia ambaye pia amewahi kumwonjesha beki Nelson Semedo wa Barcelona asali yake mnamo 2018, alianza kutambaliwa kimapenzi na Vidal mnamo Machi mwaka jana, miezi miwili tu baada ya sogora huyo wa zamani wa Juventus na Bayern Munich kutemana na kichuna Maria Teresa Matus aliyedumu naye katika ndoa kati ya 2009 na Januari 2019.

Vidal alimvisha Sonia pete ya uchumba Oktoba 2019 katika mkahawa wa Eiffel Tower jijini Paris, Ufaransa na kwa sasa wanapanga kufunga pingu za maisha.

Vidal ambaye mkataba wake na Barcelona unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu ujao wa 2020-21, anamezewa mate na Newcastle United na Manchester United nchini Uingereza.