Habari za Kitaifa

Korti yakubali mwanamume mpango wa kando alipwe asilimia 30 mali ya mwanamke

March 5th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MAHAKAMA ya Nairobi imemwagiza mwanamke amlipe mwanamume ambaye alikuwa ameishi naye kwa miaka 25, asilimia 30 ya mali zilizopatikana walipokuwa wakiishi pamoja.

Mwanamume aliyetambuliwa kama POM ili kulinda utambulisho wake, sasa atakusanya kodi kutoka kwa nyumba 11 kati ya 38 za biashara, makazi na duka, mbali na kugawiwa kodi iliyokusanywa kutoka kwa majengo hayo tangu alipofukuzwa mwaka wa 2011.

Jaji wa Mahakama Kuu Hillary Chemitei aliamuru kwamba, uamuzi wa Mahakama ya Juu uliompa mwanamume huyo asilimia 30 ya mali utekelezwe mara moja.

Mvutano huo ulitokana na kesi ya kugawanya mali hiyo ambayo ilipingwa hadi ikafika katika Mahakama ya Juu. Mahakama ya Juu ilikuwa imetangaza kwamba, hakukuwa na ndoa kati ya wawili hao lakini bado mwanamume huyo alikuwa na haki ya asilimia 30 na mwanamke asilimia 70 ya mali hiyo baada ya kupata kwamba wote walikuwa na maslahi kuihusu kisheria.

Mwanamume huyo alikuwa amewasilisha kesi dhidi ya mwanamke huyo akidai kuwa ni mke wake. Alieleza kuwa, walianza kuishi pamoja kama mume na mke mwaka wa 1986 wakaweka akiba ya pamoja benki, wakanunua mali ambayo baadaye ikawa mzozo alipofukuzwa nyumbani.

Kulingana naye, mali hiyo ilisajiliwa kwa jina la mwanamke huyo kwa sababu mmiliki aliyeuza hakutaka kumuuzia yeye kwa vile hakuwa wa kabila lake.

“Mali hiyo ilisajiliwa kwa jina la mwanamke huyo ingawa sote tulichangia kupatikana kwake,” alisema, na kuongeza kuwa walimiliki mali hiyo kati ya 1992 na 1993.Walijenga nyumba kadha wakitumia moja kama nyumba yao na kupangisha zile zingine.

Alidai kuwa, alifanya kazi zote zinazohusiana na kuunganisha umeme, maji taka na maji kwenye eneo hilo, na kuendesha baa kutoka eneo hilo. Hata hivyo alilalamika kuwa mwanamke huyo alimfukuza licha ya mchango wake. Wakati huo, alisema, kodi ilileta mapato ya Sh258,100 kwa mwezi.

Mwanamke huyo alijibu kwa kukataa madai yote ya mwanamume huyo na kusema, mwanamume huyo alikuwa tu ni rafiki yake. Alieleza mahakama kuwa, muda huo wote alikuwa na mume ambaye hawakuwa wakiishi naye pamoja, akisema alimpa tu mlalamishi jukumu la kuwa msimamizi wa biashara zake.

“Nilimruhusu kusimamia mali hiyo kwa sababu tulikuwa marafiki,” alisema.

Mahakama ilithibitisha kuwa, kwa kweli mwanamke huyo alikuwa ameolewa kwingine na hivyo basi kutaja uhusiano kati yake na mlalamishi kuwa uzinifu usioweza kutambuliwa kama ndoa. Licha ya hayo, iliagizwa mlalamishi apewe asilimia 30 ya mali zilizopatikana walipokuwa pamoja.

“Inaonekana tangu siku alipofukuzwa mwaka wa 2011, hajawahi kufaidika hata kidogo. Hakuna ushahidi wa kupinga hilo. Kwa hivyo, hakuna shaka kwamba mwanamke huyo amekuwa akifurahia kodi iliyokusanywa kutoka kwa majengo hayo tangu wakati huo,” akasema Jaji Chemitei

Mwanamume huyo alielekea Mahakama Kuu Julai 26, mwaka jana, kuomba utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Juu iliyotolewa Januari mwaka huo iliyompa asilimia 30 ya utajiri huo.

Alimuomba jaji amruhusu kuanza kunufaika na mali hiyo, kukusanya kodi na kufaidika na kodi ambayo ilikuwa imekusanywa alipokuwa ametupwa nje .

Mwanamke huyo hakuwa amewasilisha jibu lolote kufikia wakati Jaji alipotoa uamuzi huo Februari 24.