Kimataifa

Mwanamke achoka kusubiri mwanamume amtongoze, ajioa kwa harusi!

October 9th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

MWANAMKE wa miaka 32 kutoka Uganda ameshangaza ulimwengu baada ya kujifunga ndoa, kama njia ya kuepuka maswali kutoka kwa wazazi waliomtaka kuolewa.

Bi Jemimah Lulu ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Oxford aliandaa harusi hiyo ya ghafla mnamo Agosti 27, mwaka huu katika Jiji kuu la Kampala, ambapo aliwaalika marafiki zake wa karibu pekee.

Japo wageni walitarajia harusi iwe na bwana harusi, walishangaa baadae kugundua kuwa ni Bi Lulu pekee aliyekuwa bibi na ‘bwana’ harusi wa sherehe hiyo.

“Tulikuwa tukizungumza na rafiki yangu kuhusu namna wazazi walikuwa wakinisukuma kuolewa kwa muda mrefu na nilipomwelezea kuhusu wazo langu akafurahia na kujitolea kunitafutia nguo ya harusi. Niliamua kwa kuwa harusi zinaonekana za maana sana huku, nitajioa,” akasema.

Katika harusi hiyo, Bi Lulu alivalia nadhifu, akatembea hadi jukwaani kama kawaida ya sherehe hizo na hata kutoa hotuba kwa zaidi ya watu 30 waliohudhuria, akieleza sababu ya kutomhusisha mwanamume katika harusi yake.

Rafikiye mmoja naye alimlisha kiapo mwanamke huyo, ambaye alikuwa akijitolea ahadi zinazotolewa baina ya mume na mke harusini.

Inasemekana kuwa wazazi wake wamekuwa wakimtakia kupata mwanamume mzuri tangu alipokuwa na miaka 16 ili aolewe na kukaa vyema.

Hata hivyo, harusi hiyo bado haijatambulika kisheria.