Mwanamke adai Mungu alimtuma kumumunya Sh30 milioni katika sakata ya Kemsa

Mwanamke adai Mungu alimtuma kumumunya Sh30 milioni katika sakata ya Kemsa

Na SAMWEL OWINO

MWANAMKE ameshangaza kamati ya bunge inayochunguza sakata ya Sh7.8 bilioni katika Mamlaka ya Kusambaza Dawa na Vifaa vya Matibabu (Kemsa) baada ya kuwaambia wabunge kwamba ni Mungu aliyetuma kwenda shirika hilo kupata tenda ya Sh42 milioni ya kuuza vifaa vya kujikinga (PPEs).

Bi Eunice Cherono, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Leon Interior Deco and Design, aliambia kamati ya bunge kuhusu uhasibu kwamba hakujua mtu maarufu serikalini lakini ni Mungu aliyemsaidia kupata tenda ya Kemsa ya Sh30 milioni.

“Niliomba kuihusu, ni Mungu aliyenielekeza Kemsa. Naweza kusema hakika maombi yangu yalijibiwa,” Bi Cherono aliambia kamati.

“Unapoomba, unamuuliza Mungu kukufanyia kitu. Kama muumini, hauketi kitako nyumbani na kutarajia Mungu akifanyie kitu,” aliongeza Bi Cherono.

Aliambia kamati inayoongozwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir kwamba wakati wa janga la covid-19, alikuwa na matatizo ya pesa na biashara yake haikuwa inafanya vyema na akalazimika kufikiria mbinu za kuongeza mapato.

“Nilikuwa nikiendelea vibaya kwa sababu uchumi wakati huo haukuwa mzuri. Nililazimika kutafuta pesa zaidi. Naweza kufahamisha kamati huu kwamba kusema kweli sikujua yeyote,” alisema Bi Cherono.

Alikanusha kwamba alikuwa akitumiwa au alikuwa kibaraka wa mwanasiasa.

“Sikutumiwa, nawaambia hakika nilitegemea Imani na matumaini,” alisema Cherono.

“Nilienda Kemsa kwa imani kwa sababu mimi ni mwanamke anayeomba sana na kwa sababu ya hali iliyokuwa wakati huo, nilijua mahitaji ya PPEs yangekuwa ya juu. Nilijua ni Kemsa iliyohusika na vifaa hivyo,” aliongeza Bi Cherono.

You can share this post!

Raila awaonya Wapwani dhidi ya kuunda chama

Man-City watwanga Wolves na kufungua pengo la alama 15...