Habari Mseto

Mwanamke afariki baada ya kutumbukia baharini

December 24th, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

MWANAMKE alifariki Jumatano jijini Mombasa baada ya gari alilokuwa anaendesha kutumbukia baharini eneo la Kibarani.

Bi Winnie Achieng mwenye miaka 33, alikuwa na mtoto wake wa miaka 12 ambaye alinusurika kifo.Ajali hiyo ya asubuhi ilitokea baada ya Bi Achieng, aliyekuwa anaendesha gari hilo kwa kasi, kupoteza mwelekeo na kutumbukia majini.

Bi Achieng alikuwa anaendesha gari hilo aina ya Toyota Vitz kutoka upande wa Changamwe kuelekea Mombasa kisiwani.Kulingana na ripoti ya polisi, Bi Achieng alikuwa ameipita pikipiki na wakati alipokuwa anarudi mkondo wake ndipo alipogonga sehemu kando ya barabara na kupelekea gari hilo kutumbukia majini.

Kijana wake alifaulu kufungua ukanda wa usalama na kujitoa kwenye gari hilo kupitia mlango wa mbele na kuogelea kwa takriban mita 30 kabla ya kusaidiwa na watu waliokuwa wamefika kwenye eneo hilo la ajali. Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, gari hilo lilikuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi ya juu.

“Gari lilikuwa linaelekea upande wa kisiwani kwa kasi kubwa mno. Ilichukuwa muda mchache tu kuingia baharini. Nilikimbia kwenda kuwasaidia na nikaona mama huyo alikuwa amezidiwa,” akasema Bw Omar Chigamba ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufikia eneo hilo la tukio.

Alisema kuwa wakati kijana huyo alipokuwa amefanikiwa kuogelea, mamake alikuwa amekwama kwenye mkanda wa usalama wa gari na sehemu ya usukani.

Alisema kuwa mama huyo alikunywa maji mengi. na alikuwa hali taabani wakati alipotolewa kwenye gari hilo. Bi Achieng alifariki wakati alipokuwa anakimbizwa hospitalini, kulingana na ripoti za polisi.Akizungumza na Taifa Leo, babake mtoto huyo Bw Nashon Otieno alitaja kifo cha mwanamke huyo kuwa cha kusikitisha na kuwa ni pigo kwa mipango ya kifamilia waliokuwa wamepanga pamoja na marehemu.

“Mara ya mwisho kuongea na marehemu ilikuwa majuzi na tulikuwa tumepanga kuwa tutamuhamisha mtoto wetu kutoka shule aliyokuwa hadi ile nyengine ambayo ingekuwa karibu na mahali ambapo mamake ameguria hivi karibuni,” akasema.

Bi Achieng alihamia hivi majuzi eneo la Hakika Estate ambapo alikuwa anaishi na dadake Bi Beatrice Odundo.Bi Odundo alisema kuwa Bi Achieng aliondoka jana nyumbani mapema akielekea kazini katika kituo cha kuwekea mafuta cha kampuni ya Shell eneo la Bonje.

Bi Achieng amekuwa akihusika na kazi za kukusanya madeni ya kampuni hiyo kwa muda sasa.Kazi hiyo ilikuwa inamuhusisha yeye kutoka kituo kimoja hadi chengine kukusanya fedha hizo.