Kimataifa

Mwanamke afichua kuvuta bangi kila siku kulimsaidia kupunguza kilo 45

November 14th, 2018 2 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

MWANAMKE mmoja kutoka Canada amekiri kuwa kuvuta bangi kwa miaka miwili kulimfaa kupunguza uzani wa kilo 45 mwilini, akisema kuwa alipiga pafu mbili kila siku ili kupata matokeo ya kushangaza.

Bi Ayan Ikra, 28, mkazi wa Toronto alisema kuwa alipoteza uzito wa takriban kilo 45 kwa ajili ya kuvuta bangi, akisema mbeleni alikuwa mnene sana, akiwa na kilo 120.

Alisema kuwa kwa miaka kumi alikuwa amejaribu mbinu zote za kupunguza uzani kama kutumia lishe zinazopendekezwa bila mafanikio, ila tu baada ya kutumia bangi alianza kuona matokeo mema.

“Nilikuwa nikijaribu kufanya juhudi za kupunguza uzani kila wakati. Ningejaribu kwa mwezi ama miwili kisha nakata tamaa kwa kuwa sikuwa naona matunda,” akasema.

“Mnamo 2013 nilikuwa na aibu sana kuwa nilikuwa nikivaa nguo kubwa kuliko babangu. Nilikuwa na kilo 45 zaidi yake. Nilijua kuwa nilihitaji kufanya mabadiliko.”

Ni hadi Februari 2015 ndipo Ayan alijaribu kutumia kitu alichopenda kukitumia sana kuona ikiwa kingemfaa kupunguza uzani, bangi.

“Nimekuwa mpenzi wa bangi tangu kwani nilianza nilipokuwa na miaka 19. Ilinilainishia kichwa na kunifanya nijitolee kupunguza uzani. Badala ya kuivuta tu kwa burudani, niliamua kuiingiza katika ratiba yangu ya lishe,” akasema.

Alianza kuvuta misokoto miwili kwa siku kisha baada ya kuvuta angeenda kufanya mazoezi. Alisema kuwa baada ya kuvuta bangi, hakuhisi uzito wa mazoezi aliyopiga kwa saa moja kwani alikuwa mwenye nguvu tele.

“Nilianza kuivuta kabla ya chakula cha mchana na jioni ama wakati wowote nilipotaka kula ili kuepuka njaa ambayo huwa inamsababishia mtu,” akaendelea.

Alisema mwanzoni familia na marafiki hawakuelewa mbinu yake ya kipekee ya kupunguza uzani lakini walipoanza kuona matokeo wakaanza kufurahia.

Kufikia Juni 2017, alisema alikuwa amefikia uzani aliotaka wa kilo 72 na aliweza kuvaa nguo za ukubwa aliotaka.

“Hata sasa nimeanza kuvutia umakinifu wa watu wa jinsia ya kiume na mara kwa mara nimechokozwa kimapenzi mitaani,” akasema.

Alisema amefurahia hali ya kuwa mwenye uzani mdogo kwa kuwa watu wanawachangamkia watu wa aina hiyo ikilinganishwa na walio wanene.

“Ninavuta bangi kila siku na ninafurahia hivyo. Nachukia hadithi za wongo ambazo zinahusishwa na bangi. Nataka kuonyesha kuwa kuvuta bangi kunaweza kumsaidia mtu kupunguza uzani,” akasema Ayan.