Habari Mseto

Mwanamke ajiua baada ya Sh7,000 kumezwa na kamari

April 12th, 2018 1 min read

BARACK ODUOR na CHARLES WASONGA
MWANAMKE mwenye umri wa miaka 29 amejiua katika kaunti ya Homa Bay kwa kuruka kutoka kwa pikipiki ya bodaboda baada ya kupoteza pesa katika kamari.
Kisa hicho kilitokea Alhamisi jioni katika kijiji cha Kotieno Oresi katika kaunti ndogo ya Rangwe.
Inadaiwa kuwa Susan Auma aliruka kutoka kwa bodaboda hiyo iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi baada ya mumewe kumlazimisha kurejea nyumbani akikoroka baada ya kupoteza Sh7,000 katika mchezo wa kamari.
Chifu wa kata ya Kagan Magharibi Kennedy Owiti aliyethibitisha kisa hicho alisema mwanamke huyo alitoroka nyumba kwa kuhofia kuadhibiwa na mumewe baada ya kupoteza pesa hizo.
“Alikuwa anahofia kuadhibiwa na mumewe na hakutaka kurejea nyumbani hadi siku hiyo ambapo mume alianza kumsaka.
“Mumewe alimlazimisha kuabiri pikipiki ili waweze kutatua suala hilo nyumba.. lakini akiwa njia akaruka,” chifu huyo akaeleza.
Bi Auma alifariki katika Hospitali ya Rufaa ya Homa Bay alikimbizwa baada ya kupata  majeraha mabaya aliyopata kichwani na mgongoni.
Chifu Owiti alisema hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa wanandoa hao kutofautiana kuhusu mchezo wa kamari.