Habari Mseto

Mwanamke akana ulaghai wa shamba la Sh525 milioni

March 14th, 2018 1 min read

Joyce Wanjiru Nderi almaarufu Mercy Nyambura Kanyara akiwa kizimbani Jumanne kwa kosa la ulaghai wa shamba lenye thamani ya Sh525milioni. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE alishtakiwa Jumanne kwa utapeli wa shamba la ekari 15 lililo na thamani ya Sh525 milioni.

Joyce Wanjiru Nderi almaarufu Mercy Nyambura Kanyara alikabiliwa na mashtaka mawili ya ulaghai wa shamba na kumkomoa meneja wa Benki Sh3milioni.

Wanjiru alikanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Mshtakiwa alikanusha alimlaghai Bi Kanyara shamba la ekari 15 katika mtaa wa Karen kaunti ya Nairobi lenye thamani ya Sh525,000,000 mnamo Novemba 9 2017.

Akitumia hati za shamba hilo , Wanjiru , alishtakiwa alimlaghai Bw Martin Matu Githua Sh3milioni akidai hati miliki ya shamba hiyo ya Bi Kanyara ilikuwa yake.

Alipokea pesa hizo kutoka kwa benki ya  Federal Investments Limited iliyoko Nairobi.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh800,000 pesa tasilimu. Kesi itasikizwa Aprili 9