Habari za Kaunti

Mwanamke akanusha kuiba pombe ya mzinga chupa mbili

May 18th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE ambaye inadaiwa alinaswa na kamera za siri akiiba pombe kali katika duka lililoko Two Rivers, alimlilia hakimu asiagize azuiliwe katika gereza la Lang’ata, akidai hana mtu wa kuwatunza watoto wake akiwa gerezani.

Bi Lilian Makena alimlilia hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi amwonee huruma kwa vile “mimi ni mama na hakuna mtu wa kunitunzia watoto wangu endapo nitafanywa mahabusu katika gereza la Lang’ata.”

Bi Makena aliyekana kuiba pombe kali aina ya Hennesy XO yenye thamani ya Sh88,000 aliomba aachiliwe kwa dhamana isiyozidi Sh10,000.

“Nakusihi Mheshimiwa uniachilie kwa dhamana isiyozidi Sh10,000. Mimi niko na watoto wawili ninaowachumia na ukiamuru nilipe kiwango cha juu kuliko dhamana hiyo, nitaozea jela tu,” aliomba Bi Makena.

Mshtakiwa alieleza hakimu kwamba siku anayodaiwa aliiba pombe kali hiyo, alikuwa amelazwa hospitalini.

Bi Makena alimkabidhi Bw Ochoi nakala ya rekodi ya hospitali alikokuwa amelazwa.

“Je, umeona ripoti hii ya hospitali ya mshtakiwa,” Bw Ekhubi alimuuliza kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki.

Bi Kariuki alieza mahakama kwamba polisi walimtambua mshtakiwa baada ya kukagua na kuchambua picha za video zilizonaswa na kamera za siri katika duka hilo la Supa la Two Rivers.

“Mimi sina kazi rasmi na mapato yangu ni haba. Sina njia ya kupata dhamana ya kiwango cha juu,” Bi Makena alieleza hakimu akiomba dhamana.

Hakimu alimwamuru afisa anayechunguza kesi hiyo afike katika hospitali ambapo mshtakiwa alikuwa amelazwa kubaini ugonjwa anaougua.

Bi Lilian Makena Mwenda akiwa katika mahakama ya Milimani aliposhtakiwa kuiba chupa mbili za pombe ya mzinga ya thamani ya Sh88,000. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Bw Ekhubi alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh50,000.

Pia aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa pamoja na watu wa familia yake kisha iwasilishe ripoti kortini.

“Ikiwa ulikamatwa na polisi baada ya kamera za siri kukunasa ukiiba, basi itabidi ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia iwasilishwe kabla ya ombi lako la kuachiliwa kwa dhamana ya kiwango cha chini kutiliwa maanani,” Bw Ekhubi alimweleza mshtakiwa.

Mahakama pia iliamuru idara ya urekebishaji tabia ibaini idadi ya watoto wa mshtakiwa kabla ya ombi lake kutiliwa maanani.

Kesi hiyo itatajwa Mei 30, 2024, kutengewa siku ya kusikilizwa.

Bi Makena alikabiliwa na shtaka la kuiba chupa mbili za pombe ya mzinga aina ya Hennesy XO yenye thamani ya Sh88,000 mnamo Aprili 28, 2024.

Inadaiwa aliiba pombe hiyo kutoka duka la Whisky Liquor Shop lililoko Two Rivers Mall eneo la Westlands, Nairobi.

Alishindwa kulipa dhamana hiyo na kupelekwa gereza la wanawake lililoko Lang’ata, Nairobi.