Habari Mseto

Mwanamke alilia polisi waachilie mume aliyenajisi binti yake

June 14th, 2018 1 min read

Na DERICK LUVEGA

MWANAMKE mmoja alishangaza wakazi wa Kaunti ya Vihiga alipowalilia polisi wamwachilie mumewe aliyekamatwa na kuzuiliwa kwa kumnajisi binti yake mwenye umri wa miaka 11. Msichana huyo ni binti ya mwanamke huyo na binti ya kambo wa mshukiwa.

Mwanamke huyo, 27, alisema ni mjamzito na anatarajia kujifungua mwezi ujao akiwa karibu na mumewe.

Mwanamke huyo ambaye ni mama ya watoto watatu, aliambia polisi kwamba wanafaa kumwachilia huru mumewe bila masharti kwa sababu ya hali yake. Mkuu wa polisi eneo la Vihiga (OCPD) Bw Justin Nyagah, alithibitisha kuwa mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Vihiga na atashtakiwa kwa unajisi na kushiriki kitendo cha aibu na mtoto.

Lakini mama huyo anayetoka kijiji cha Wangombi aliwaomba polisi kumsamehe mumewe akisema hana mtu mwingine wa kumsaidia. Alisema familia yake ilikataa kumpokea na kumfukuza akachanganyikiwa.”Watu hutenda makosa. Ninakubali mume wangu alitenda makosa lakini anafaa kusamehewa,” alisema.

Aliendelea: “Iwapo atarudia makosa, basi ashtakiwe. Niko na mimba na nitajifungua mwezi ujao. Ninataka kuwa karibu na mume wangu. Nitafanya nini akifungwa jela.”

“Wazazi wangu ni masikini. Baba yangu ni mgonjwa. Nina mtoto mwingine nyumbani kwa wazazi wangu. Tayari ndugu yangu amenionya nisirudi kwa wazazi wangu,” alisema. Akionekana kutamauka, mwanamke huyo alilia polisi wamwachilie mumewe ili waendelee kuishi pamoja kwa sababu hana pa kwenda.

Hata hivyo, Bw Nyagah alisisitiza kuwa ni lazima mshukiwa afikishwe kortini.

“Tulipata ripoti kwamba msichana huyo alinajisiwa na baba yake. Tulimpeleka hospitali na ripoti iko tayari. Tuko tayari kumfungulia mashtaka,” alisema.