Kimataifa

Mwanamke alipiga hadi kuua bintiye wa miezi 7, korti yaambiwa

July 24th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMKE kutoka London, Uingereza yuko hatarini kutupwa jela, baada ya kumpiga bintiye wa miezi saba hadi kufa.

Kinaya ni kuwa mwanamke huyo ameishi miaka akitamani kujifungua, kwa njia ya IVF.

Shalina Padmanabha, 33, anatuhumiwa kuwa amekuwa akimchapa bintiye miezi mitatu iliyopita, baada ya kukaa miezi minne hospitalini tangu alipojifungua.

Mahakama iliambiwa jinsi Shalina na mumewe walijaribu kutafuta mtoto, kabla ya kufanikiwa na akajifungua Februari 2017.

Lakini mwanawe alizaliwa na matatizo ya kiafya, ambayo yalimlazimu kukaa hospitalini kwa miezi minne akitibiwa. Korti ilielezwa mshukiwa alianza kumdhulumu mtoto huyo tangu alipokuwa hospitalini, akimpiga kichwani ama kukigongesha.

Lakini baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani, mshukiwa anadaiwa kuendelea kumpiga mtoto huyo, hadi akafa.

Shalina alilia alipokuwa kizimbani, japo korti ilimwondolea kosa la mauaji na kumfungulia la kuua bila kukusudia, na kumdhulumu mtoto wa chini ya miaka 16.

Majaji waliambiwa mtoto huyo alifariki katika hospitali moja Agosti 2017, kutokana na majeraha mabaya aliyopata kichwani.

Alipokamatwa mwaka huo, aliambia polisi kuwa mtoto huyo alikuwa na nguvu sana na aliyekuwa amejikunja.

Maiti ya mtoto huyo ilipofanyiwa upasuaji, ilibainika kuwa alikuwa na majeraha kichwani, kwenye mbavu na macho, ambayo yalikuwa yakivuja damu.

Mwanamke huyo atahukumiwa Julai 19.