Makala

Mwanamke aliyeangamia Shakahola na mtoto alitafuta mhubiri wa kufufua mumewe

March 28th, 2024 3 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

SIMANZI ilitanda katika kijiji cha Radienya, eneobunge la Nyatike, Kaunti ya Migori mnamo Alhamisi wakati wa mazishi ya Bella Ouma na bintiye Lisa, ambao walikuwa miongoni mwa watu walioaga dunia kwa mfungo tata msituni Shakahola.

Familia iliyofiwa hata hivyo haijatulia kwa sababu binti mwingine wa Bi Ouma bado haijulikani aliko.

Kulingana na Bi Norah Akoth, shemeji yake–Bella–aliondoka kijijini mwaka 2019, siku moja baada ya kumzika mumewe. Alisema kuwa alikuwa akienda jijini Nairobi.

Bi Akoth aliambia Taifa Leo kuwa Bella alipokea simu kutoka kwa mtu ambaye alimtaka kubeba suti moja ya marehemu mumewe kwa lengo la kuipeleka kwa mchungaji mmoja ambaye angemwombea ili mumewe afufuke.

“Baada ya mazishi ya kaka yangu, shemeji yangu aliondoka kimyakimya na watoto wake wawili wa kike. Nilipompigia simu kumuuliza alikokuwa, aliniambia kuwa alikuwa ameabiri basi la kuenda Nairobi ambako angemuona Yesu,” Bi Akoth alisema akiwa nyumbani kwao Radienya.

Alisema familia ilistaajabishwa na matamshi ya Bella.

“Aliniambia alikuwa amebeba suti moja ya marehemu mumewe kwa maombi, ambayo yangemfanya afufuke,” akasimulia.

Inasemekana Bella, alionyesha dalili za itikadi kali wakati wa mazishi ya mumewe.

Shemeji mwingine wa Bella, Bw Philip Ochola alisema aligombana na baba mkwe wakati wa mazishi ya mumewe.

“Aligombana na baba yangu wakati wa mazishi ya mumewe ambaye ni ndugu yangu. Alisisitiza kwamba watu wa kanisa lake wanapaswa kudhibiti kikamilifu mpango wa mazishi. Hata hakutaka kumsikiliza baba yangu alipojaribu kumtuliza,” akasema Bw Ochola.

Familia hiyo aidha ilifichua Bella aliwahi kupiga simu nyumbani kuwajulisha kwamba alikuwa amejiunga na kanisa la mchungaji Paul Mackenzie alikoenda kutafuta wokovu.

Bi Akoth alisema binti mdogo wa Bella alizaliwa na ugonjwa fulani na kwamba watu wa kanisa lake waliahidi kumsafirisha kwa ndege hadi nchini India kwa matibabu maalum.

Kwa kuwa Bella alitoka haraka nyumbani bila hata kuwapasha habari, “hatukuwa na jingine isipokuwa kumtakia kila la heri katika shughuli zake”.

Lakini habari zilipozuka kwamba miili ya watu ilikuwa imegunduliwa katika msitu wa Shakahola mnamo 2023, familia hiyo iliingiwa na wasiwasi.

Bw Ochola alisema waliingiwa na tumbojoto.

“Tulijaribu kumtafuta kwa simu, lakini juhudi zetu zote ziliambulia patupu. Tulilazimika kutuma mmoja wetu Kilifi kuwaangalia,” Bw Ochola akaeleza.

Ni hapo ndipo mwili wake ulipatikana.

“Habari tulizo nazo ni kuwa Bella alikuwa miongoni mwa waliopatikana wakiwa wamejificha ndani ya msitu wa Shakahola wakiwa wamefunga kwa imani kuwa hiyo ndio njia pekee ya kukutana na Yesu. Alipelekwa hospitalini lakini baadaye alifariki dunia. Tuliambiwa binti wake mkubwa alifukuliwa kutoka kwa makaburi msituni humo lakini hatujui mtoto mwingine yuko wapi,” akaeleza.

Bw Ochola alisema habari za Bella na bintiye Lisa zilipodhihirika, walifanya mikesha ya usiku hadi mwezi mmoja.

Lakini kwa vile mchakato wa kupata miili yao ulichukua muda mrefu kuliko jinsi walivyotarajia, hivyo wakaamua kurudi majumbani mwao.

“Sisi ni familia kubwa hapa. Baadhi ya ndugu zangu hawaishi hapa. Ilikuwa vigumu kwetu kuendelea kukesha hapa, kwani hatukujua ni lini tungepata miili,” akasema.

Alibainisha kuwa kama familia, walitumia rasilimali nyingi baada ya mkasa huu kuwakumba.

“Hatuwezi kutaja kiasi halisi cha fedha ambacho tumetumia katika hili, lakini tumebaki hoi kifedha. Hatujaona msaada wowote kutoka kwa serikali isipokuwa kutoka kwa marafiki na wasamaria wema ambao wamesimama pamoja nasi,” akasema.

Baada ya serikali kutangaza kwamba familia zilizoathiriwa sasa zitaanza kupokea miili ya mauaji ya Shakahola, Bw Ochola alisema wanafamilia walichanga pesa kuwezesha usafirishaji wa miili hiyo kutoka Malindi hadi Migori.

Safari yao kutoka Malindi ilianza Jumatano, saa kumi na moja kasorobo jioni. Walifika kijijini Radienya mnamo Alhamisi saa nane na robo.

“Kifamilia tumeumia sana, kizazi cha kakangu kimefutika kabisa, hatujui yule binti mwingine yuko wapi, lakini tukiambiwa mwili wake umepatikana ni sawa… tutakwenda kumchukua na kuleta mwili nyumbani kwa mazishi,” Bi Akoth akasema.

Maoni ya Bi Akoth yaliungwa mkono na kakake– Bw Ochola.

“Tunathamini watu wetu. Tulikuwa tumekatishwa tamaa sana na baadhi ya watu waliokuwa wakituambia tuache miili hiyo huko lakini tukasema tutafanya kila tuwezalo ili kuwapa heshima zao,” Bw Ochola akasema.

Bw Ochola na dadake Bi Akoth waliambia Taifa Leo kwamba familia yao ililelewa katika Kanisa la Kiadventista.

“Sisi ni wa madhehebu tofauti. Tuna Waadventista na Wakatoliki katika familia hii. Mimi mwenyewe ni Mwislamu, lakini hatujawahi kuwa na mtu yeyote wa familia yetu anayejihusisha na madhehebu ya itikadi kali,” Bw Ochola akasema.

Miili hiyo miwili ililetwa katika kijiji cha Radienya ikiwa katika sanduku moja la mbao. Walikuwa wamefungwa juu ya gari kwa karatasi nyeusi ya nailoni.

Majeneza mawili yaliletwa baadaye na kila maiti kuwekwa ilale kivyake.

Kulikuwa na hotuba fupi kutoka kwa jamaa.

Maombi na nyimbo za kutuliza zilipewa muda mwingi.

Waliopata nafasi ya kusema neno, walisema pole kwa familia. Walimwomba Mungu asiruhusu jambo lililoikumba familia hiyo litokee kwa mtu mwingine yeyote.

Wito ulitolewa kwamba mchungaji Mackenzie na washirika wake wanaodaiwa kusababisha maafa hayo, wakabiliwe vilivyo kisheria.

Mazishi yalikuwa matulivu sana. Ni waombolezaji wachache tu waliohudhuria, wengi wao wakitoka upande wa kwa kina Bella.