Habari za Kitaifa

Mwanamke aliyedaiwa kuanguka aliuawa kabla mwili wake kurushwa – Polisi

January 20th, 2024 1 min read

NA JOSEPH NDUNDA

UCHUNGUZI wa polisi unaonyesha mwanamke ambaye awali iliripotiwa kwamba aliaga dunia baada ya kuruka kutoka kwa orofa ya tatu ya jengo la Ascot lililoko Langata, Nairobi, aliuawa na mwili wake kutupwa nyuma ya jengo hilo.

Ripoti ya upasuaji ilionyesha kwamba Nelvine Museti aliaga dunia kutokana na majeraha ya kichwani kutokana na kifaa butu.

Mwili wake ulipatikana damu ikitoka puani.

Mnamo Januari 11, 2024, majirani walisikia mwanguko kwa kishindo saa kumi na moja asubuhi na saa moja baadaye, mwili wake ukapatikana.

Tukio hilo liliripotiwa na mtunzaji wa nyumba hizo za wapangaji.

Polisi walipofika hapo, walipekua nyumba ya marehemu ambayo haikuwa imefungwa.

Kwenye hati ya kiapo katika Mahakama ya Kibera, konstebo Johnson Wanjohi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Langata, alisema polisi walipata kondomu, ishara kwamba, Museti alikuwa na mwanamume usiku wa kuamkia siku hiyo.

Pia walipata chupa ya bia, glasi mbili zinazoaminika zilikuwa za pombe, bangi na chupa ya soda ikiwa imejaa nusu.

“Pombe na soda ilipatikana juu mezani katika nyumba hiyo na pia kondomu iliyotumika ilikuwa kwa nyumba,” akasema Bw Wanjohi.

Vitu hivyo vimepelekwa kwa maabara ya serikali kufanyiwa uchunguzi wa DNA, kwa mujibu wa DCI.

Sasa maafisa wamesema wanachunguza uhalifu unaohusu mauaji kwa mujibu wa kipengee cha 203 kama kinavyorejelewa pamoja na sehemu ya 204 ya Kanuni za Adhabu.

Upelelezi wa DCI ulifanikisha kukamatwa kwa polisi wa kutoka kitengo cha GSU katika makao makuu ya Ruaraka, Nairobi.

Bw Victor Otieno Ouma kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Langata baada ya Konstebo Wanjohi kupewa agizo la kumzuilia kwa siku 21. Agizo lilitolewa na Hakimu Mwandamizi Mkuu Irene Kahuya.

Maafisa wa DCI walisema mawimbi ya mawasiliano ya simu katika simu ya marehemu yaliwaelekeza kwa Bw Ouma kama mshukiwa wa mauaji hayo.