Habari za Kitaifa

Mwanamke aliyefanya hakimu apigwe risasi alikosa vikao 7 vya korti


MWANAMKE ambaye alisababisha Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Makadara Monica Kivuti apigwe risisi, alikuwa amekosa vikao vya korti mara saba.

Bi Kivuti alikuwa akisikiza kesi ambapo Bi Wairimu alikuwa ameshtakiwa kwa kupokea Sh2.9 milioni kwa njia ya ulaghai.

Rekodi ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) inaonyesha kuwa Bi Wairimu alikamatwa Septemba 19, 2022 na alikuwa nje kwa dhamana ya polisi.

Aliamrishwa afike kortini mnamo Oktoba 24, 2022 lakini akakosa kufika. Kesi hiyo iliratibiwa kutajwa mnamo Novemba 23, 2022 lakini hakufika tena kortini ili ashtakiwe.

Aliendelea na mtindo huo ambapo alikosa vikao vya kesi mnamo Machi 7, Mei 9 na Disemba 5, 2023. Hatimaye alifika Januari 5 na akakanusha mashtaka dhidi yake na akaachiliwa kwa dhamana.

Mnamo Mei 4, Bi Wairimu alihitajika kufika kortini ambapo kesi hiyo ilitajwa lakini hakufika. Hapo ndipo korti ilitoa amri akamatwe na dhamana yake ifutwe.

Pia alikosa kusikizwa kwa kesi hiyo mnamo Mei 13 na Mei 30, 2024.

Kesi hiyo ilipotajwa mnamo Mei 30 alikosa tena kufika na wakili wake akawasilisha stakabadhi za kimatibabu ambazo zilionyesha kuwa alikuwa mgonjwa.

Wakati wa vikao hivi vyote aliyewasilisha kesi akidai alihadaiwa hela alikuwa kortini na alilalamikia hatua ya Wairimu kukosa vikao vya korti.

Wakili ahoji uhalali wa stakabadhi

Wakili wa mshtakiwa alihoji uhalali wa stakabadhi hizo za kimatibabu lakini hakimu akaamrisha afisa wa uchunguzi kuthibitisha iwapo zilikuwa halali.

Siku ya tukio, Juni 13, Bi Wairimu alifika kortini na afisa wa uchunguzi aliwasilisha ripoti kortini iliyosema stakabadhi za kimatibabu alizokuwa amewasilisha hazikuwa halali.

Ni kwa msingi huo ambapo Bi Kivuti aliamrisha azuiliwe korokoroni. Kupitia mawakili wake, Bi Wairimu aliiomba mahakama msamaha kwa kutoa habari zisizo za kweli kuhusu matibabu yake na akaomba dhamana yake isiondolewe.

Hata hivyo, Bi Kivuti alikumbatia hoja ya Bi Wairimu kutohudhuria vikao vya kesi na akaamrisha azuiliwe katika gereza la wanawake la Kibera.

Ni uamuzi huo ndio ulisababisha Samson Kipchirchir Ruto, mumewe mshtakiwa kumpiga risasi.