Habari Mseto

Mwanamke aliyejifungua watoto 5 afariki

April 7th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MWANAMKE kutoka kijiji cha Sisokhe eneo bunge la Navakholo, kaunti ya Kakamega ambaye mwezi Machi alijifungua pacha watano kwa mpigo alifariki Jumapili.

Na wawili kati ya watoto hao (wa kiume) pia walifariki majuma mawili yaliyopita, baada ya kukumbwa na matatizo ya kupumua.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret, Bw Wilson Arwasa, Evelyn Namukhula, 28 alianza kulalamikia maumivu ya kifua mwendo wa saa nne za usiku Jumamosi.

Baadaye, Bw Arwasa akasema, Bi Namukhula, alifariki Jumapili alasiri katika hospitali hiyo ambako amekuwa akihudumiwa pamoja na wanawe watano.

Bi Namukhula aligonga vichwa vya habari alipoandikisha historia kwa kujifungua watoto watatu wa kike na wawili wavulana kwa njia ya upasuaji katika Hospitali Kuu ya Kakamega.

Baada ya siku kadhaa, alihamishwa hadi MTRH mjini Eldoret baada ya mtoto mmoja kukumbwa na matatizo ya kupumua.

“Mtoto wangu alipata changamoto za kupumua na madaktariwa Hospitali ya Kakamega wanaamua kutuhamishia hapa ili mtoto huyo wa kiume apewe hudumu za kumwezesha kupumua,” akawaambia wanahabari katika hospitali hiyo.

Bw Arwasa alisema watoto japo watoto wawili walifariki, wale wengine watatu, wa kike, wako katika hali nzuri.

Wahudumu wa afya katika MTRH walisema kuwa watoto wengine wanne walikuwa katika hali nzuri japo hawakuwa wameanza kunyonya.

Mtoto mdogo zaidi miongoni mwao alikuwa na uzani wa gramu 840 walipozaliwa ilhali uzani wa wastani unapasa kuwa kilo 3.5.

Marehemu na mumewe, Herbert Wawire, wamebarikiwa na watoto wengine wanne. Bw Wawire huchuma mapato kwa kufanya kazi za sulubu kijijini Sisokhe.