Kimataifa

Mwanamke aliyetupwa ndani kwa kumtusi Museveni aachiliwa

February 20th, 2020 1 min read

Na DAILY MONITOR

MAHAKAMA nchini Uganda imemwachilia huru mwanaharakati Dkt Stella Nyanzi ambaye alikuwa amefungwa jela miaka 18 Agosti mwaka jana kwa kumtusi Rais Yoweri Museveni.

Jaji Peter Henry Adonyo wa kitengo cha uhalifu wa kimataifa katika Mahakama Kuu alisema mahakama ya ngazi ya chini haina mamlaka ya kumtuhumu Dkt Nyanzi kwa kumdhulumu Museveni kupitia jumbe za mitandaoni.

“Upande wa Mashtaka haukuthibitisha aina ya kifaa kilichotumiwa kutuma habari hizo kupitia mitandaoni,” jaji huyo akasema.

Mahakama hiyo pia ilisema kuwa kundi la mawakili wa Dkt Nyanzi hawakupewa muda wa kutosha kujiandaa. Vile vile, shahidi wa upande wa mashtaka hakutoa ripoti ya kuonyesha kuwa Dkt Nyanzi alitenda kosa hilo.

Jaji Adonyo baadaye alitoa amri kwa Dkt Nyanzi ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Museveni aachiliwe huru mara moja, hatua ambayo ilichangamkiwa na watu waliokuwa mahakamani.

Lakini taharuki na wasiwasi ilishuhudiwa katika mahakama hiyo pale Dkt Nyanzi alipozirai alipokuwa akisadiwa kutia saini stakabadhi ya kumwachilia huru. Iliwabidi askari jela kumbeba na kumwenda ndani ya gari lao na wakaondoka.

Alirejeshwa katika gereza la wanawake la Luzira ili apumzike kabla ya kuruhusiwa kuondoka.

Mnamo Septemba 2018, Dkt Nyanzi alichapisha shairi iliandikwa kwa maneno machafu ya kumkosea heshima Museveni na mamake mzazi akimlaumu kwa utawala wa kidhalimu kwa zaidi ya miaka 30.

Tafsiri: CHARLES WASONGA