Habari Mseto

Mwanamke amuua mwanamume aliyemzaba kofi

July 24th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMKE Jumanne alimuua mwanamume katika eneo la Elburgon, Kaunti ya Nakuru, baada ya mwanamume huyo kumzaba kofi.

Kulingana na walioshuhudia, mwanamke huyo kwa jina Margaret Wambui,34 alimdunga kisu na kumuua mwanamume huyo, baada ya marehemu kumzaba kofi.

Wawili hao wanasemekana kuwa walikuwa wakizomeana ndipo marehemu, Benson Chege, 32 akamzaba kofi Bi Wambui, lakini Bi Wambui naye akachukua kisu na kumdunga.

“Marehemu alimzaba kofi Bi Wambui ndipo naye akakasirika na kuchukua kisu akamdunga mara moja,” akasema mkazi ambaye alishuhudia.

Kamanda wa polisi eneo la Molo Isaac Odumbe alisema polisi walimpata marehemu akiwa amelala huku damu ikimzingira katika duka la nyama mjini Elburgon Jumanne usiku.

Walijaribu kumkimbiza hospitalini lakini akathibitishwa kufa punde tu alipofikishwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Elburgon.

Bw Odumbe alisema mwanamke huyo alikamatwa mara moja na kuwa anazuiliwa na polisi, akisubiri kufikishwa kortini.

Alisema polisi walipata kisu kilichotumika katika mauaji kando ya mwili wa marehemu.

Kufuatia kisa hicho, wakazi walipandwa na hasira na walikuwa wakitaka kumvamia mshukiwa, lakini polisi wakafika na kumuokoa.