Habari Mseto

Mwanamke amuua mwizi aliyejaribu kumbaka

May 23rd, 2019 1 min read

Na NICHOLAS KOMU

Mwanamke mmoja Alhamisi alimuua kwa kumdunga kisu mwanamume aliyevunja na kuingia katika kioski chake katika mtaa wa Ngangarithi mjini Nyeri.

Polisi walisema kwamba mwanamke huyo alikuwa akijilinda baada ya mwanaume huyo kujaribu kumbaka wakati wa kisa hicho kilichotokea saa tisa alfajiri.

Mwanamume aliyeuawa ambaye hakutambuliwa, alikuwa ameandamana na mwenzake kuvunja kioski hicho kilichoko Ngangarithi Centre.

Inaaminika kuwa wawili hao walitaka kuiba mali kutoka kioski hicho kinachotumiwa kuuza aina tofauti za mboga. Polisi walisema kwamba wezi hao walikuwa tayari wameiba bidhaa za zaidi ya Sh50,000 kabla ya njama yao kutibuliwa.

Jirani aliyesikia wakivunja kioski alimpigia simu mmiliki wa biashara hiyo kumfahamisha mali yake ilikuwa ikiibwa. Katika juhudi za kuokoa mali yao mwanamke huyo na mumewe walioomba tusiwataje majina kufuatia yaliyojiri, waliamua kukabiliana na wezi hao.

“Mke wangu aliniita na kunifahamisha kwamba kuna watu ambao walikuwa wamevunja kioski anakofanyia biashara. Tuliondoka nyumbani kwenda kuangalia,” alisema mume wa mwanamke huyo.

Walipowasili katika kioski kilichoko mita chache kutoka nyumba yao, wezi hao walikimbia na mumewe akawakimbiza na kuacha mkewe ndani ya kioski kuchunguza mali iliyokuwa imeibwa.

Ripoti ya polisi inasema kwamba mmoja wa wezi hao aliyekuwa amejificha kwenye kioski kilichokuwa karibu alimshambulia mwanamke huyo, mumewe alipokuwa akiwafuata wezi waliotoroka.