Kimataifa

Mwanamke amuua na kumpika mpenziwe wa miaka 7

November 22nd, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

MWANAMKE mmoja kutoka Morocco ameshangaza ulimwengu baada ya kudaiwa kumuua kisha kumpika mpenzi wake.

Mwanamke huyo ambaye ameshtakiwa kumwangamiza  mpenzi wake huyo anadaiwa kupika mlo kisha kuuzia wafanyakazi kutoka Pakistan ambao wako UAE, kumbe ulikua mwili wa mpenzi wake.

Viongozi wa mashtaka wamesema kuwa mwanamke huyo alimuua mpenzi wake miezi mitatu iliyopita, japo kisa hicho kilijulikana majuzi baada ya jino la binadamu kupatikana katika mashine yake ya kuandaa vyakula.

Baadaye, mshukiwa huyo amedaiwa kukiri kwa polisi kutenda kosa hilo, akisema ulikuwa ‘wakati wa uwazimu’, gazeti moja la taifa hilo liliripoti.

Uchunguzi unaendelezwa kuhusiana na kisa hicho na baada yake kukamilika mshtakiwa ambaye yuko miaka ya 30 atafunguliwa mashtaka.

Ripoti zilisema kuwa alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na marehemu kwa miaka saba.

Anadaiwa kumuua baada ya mwanaume huyo kumjulisha kuwa alipanga kumuoa mwanamke mwingine kutoka Morocco.

Japo polisi hawakusema namna alivyotekeleza mauaji, walisema kuwa aliandaa viungo vya mwili wa marehemu pamoja na wali wa kitamaduni na kuwauzia wafanyakazi wa Kipakistani waliokuwa wakifanya kazi karibu.

Inasemekana kuwa ukweli ulijulikana tu baada ya kakake marehemu kwenda kumtafuta walipokuwa wakiishi na kupata jino la binadamu katika mashine ya blender.

Mwanaume huyo alifika kwa polisi kuripoti kupotea kwa nduguye ndipo uchunguzi wa DNA ukafanyiwa jino na kufahamika kuwa lilikuwa la marehemu.

Polisi wamesema kuwa mwanamke huyo kwanza alimhadaa kakake marehemu kuwa alimfukuza huko nyumbani, lakini baadaye akazirai na kukiri alipokuwa akihojiwa na polisi.

Baada ya kumuua anadaiwa kutafuta msaada wa rafikiye kungarisha nyumba.

Mshukiwa sasa ametumwa hospitalini kupimwa akili kabla ya kufunguliwa mashtaka.