Makala

Mwanamke anayeandamwa na kesi za mauaji zinazohusu ‘penzi kwa wazungu’

January 18th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Milimani mnamo Jumatano iliamuru polisi wawasilishe ripoti ikiwa mwanamke raia wa Rwanda anayeshtakiwa kupanga njama za kumuua mpenziwe raia wa Uswisi amewahi kuwa na pasipoti.

Hakimu mwandamizi Bi Martha Nanzushi alimwagiza afisa anayechunguza kesi inayowakabili Antoinette Uwineza almaarufu Dardeh PM Kanswen na nduguye Eddy Kwizera, afike katika ubalozi wa Rwanda jijini Nairobi na idara ya uhamiaji kubaini ikiwa wawili hao wamewahi kuwa na vyeti vya usafiri.

Bi Nanzushi aliamuru kesi hiyo itajwe Januari 23, 2024, ripoti iwasilishwe kuhusu pasipoti ya Uwineza ambaye aliwahi shtakiwa kumuua mwanamke mwingine raia wa Rwanda waliyekuwa wakimng’ang’ania mwanamume mzungu.

Mnamo Novemba 1, 2018, Uwineza alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani na Jaji Jessie Lesiit (ambaye sasa ni jaji mahakama ya rufaa) kwa kumuua Winnie Uwambaye pamoja na mwanaye wa miezi saba.

Uwineza na Uwambaye walikuwa wanang’ang’ania mpenzi wao Mzungu.

Baada ya kumuua Uwambaye kwa karatasi ya nailoni, Jaji Lesiit alisema Uwineza alifunga maiti za wawili hao kwa shuka ya lojing’i na kutoroka.

Polisi walimtia nguvuni Uwineza katika mtaa wa Kayole akiwa na simu ya Uwambaye.

“Mauaji ya Uwambaye yalikuwa ya kinyama. Uwineza alikuwa amepanga kuwatoa uhai mama na mwanawe,” alisema Jaji Lesiit akipitisha adhabu.

Maiti ya Uwambaye ilipatikana mnamo Februari 16, 2013, katika hoteli ya Saharan Lodge iliyoko barabara ya Duruma, Nairobi.

Marehemu alikuwa na umri wa miaka 42 alipokumbana na mauti hotelini.

Alinyongwa kwa karatasi ya nailoni.

Mwanamume waliyekuwa wameshtakiwa naye Uwineza aliachiliwa kwa kukosekana ushahidi.

Lakini Septemba 2020 Jaji Mkuu Martha Koome alipokuwa jaji wa mahakama ya rufaa pamoja na majaji Hannah Okwengu na Fatuma Sichale walimwachilia huru Uwineza wakisema “upande wa mashtaka haukuthibitisha ni yeye alimuua Uwambaye.”

Mnamo Desemba 31, 2023, maafisa wa uchunguzi wa jinai walimtia nguvuni Uwineza na nduguye Kwizera katika eneo la Brookside liloko Westlands, Nairobi walipokuwa wamefaulu kumpeleka raia huyo wa Uswisi Helbling Guico Paul (mpenziwe Uwineza).

Shtaka dhidi yao linasema mnamo Desemba 30, 2023, Uwineza alipanga jinsi ambavyo angemuua Paul kisha akawatafuta wauaji.

Ilitokea kwamba Uwineza alikuwa ametafuta watu ambao baadaye walijitambulisha kuwa p0lisi na wakamkamata.

Sasa Uwineza na Eddy wameshtakiwa kula njama za kumuua Paul na kumwibia Euro 850.

Mwanamke raia wa Rwanda Antoinette Uwineza (kushoto) akiwa na kaka yake Eddy Kwizera katika Mahakama ya Milimani mnamo Januari 17, 2024, kwa maelekezo kuhusiana na kesi ya kupanga njama ya kumuua mpenzi wake, raia wa Uswisi Helbling Guico Paul mnamo Desemba 30, 2023. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Akihojiwa na polisi, Uwineza alionyesha taarifa ya benki ikionyesha kati ya Machi 17 na Juni 10, 2023, alikuwa amepokea kitita cha Sh9.2 milioni kutoka kwa Paul.

Uwineza na Eddy walikana mashtaka mawili dhidi yao.

Wakimshawishi Paul afike nchini, Uwineza alikuwa amemshawishi angemuuzia dhahabu.

Upande wa mashtaka unaoongozwa na Bi Judy Ingutia ulieleza Bi Nanzushi kwamba njama za kumuua Paul zilipangwa Desemba 30, 2023.

Mauaji yalikuwa yatekelezwe mkesha wa Mwaka Mpya katika eneo la Brookside, Westlands, Nairobi.

Washtakiwa walikuwa wamekodisha chumba ambapo Paul angemaliziwa.

Lakini Mswisi huyo mwenye bahati kama mtende aliokolewa na polisi kabla ya kuangamizwa.

Mahakama ilielezwa washtakiwa walipatikana wakiwa na mifuko ya nailoni, visu na tembe sita za dawa ya kulevya aina ya Nitrest.

Bi Nanzushi alikuwa amemwamuru Uwineza afike kortini kuwasilisha pasipoti ili ithibitike yeye ni raia wa Rwanda na alikuwa na stakabadhi zote.

Waliposhtakiwa mahakama iliwaachilie kwa dhamana ya Sh200,000 pesa taslimu ama wawasilishe mdhamini wa Sh500,000.

Uwineza alifaulu kulipa dhamana ya Sh200,000 lakini Eddy alishindwa.

Eddy anazuiliwa katika gereza la Industrial Area.

Kesi hiyo itatajwa Januari 23, 2024.

Wawili hao wamekanusha mashtaka dhidi yao.

Wakili John Swaka anayewatetea wawili hao aliomba muda Uwineza awasilishe stakabadhi za kuthibitisha yuko na pasipoti lakini ilipotea na sasa anatumia Visacard.

Bw Swaka alimweleza hakimu Rais William Ruto ameondolea masharti kwamba wageni waingie nchini Kenya wakiwa na viza.