Habari Mseto

Mwanamke apatikana na hatia ya kuua mumewe na kukatakata mwili

October 12th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE amepatikana na hatia ya kumuua mumewe kisha akaukatakata mwili wake vipande vipande na kuupakia ndani ya mfuko kisha akautupa ndani ya timbo la mawe katika kaunti ya Machakos.

Jaji Stellah Mutuku alimpata na hatia Mary Njoki Ng’ang’a ya kumuua kinyama mumewe James Ng’ang’a Ritho aliyekuwa na umri wa miaka 60.

Mary alikabiliwa na shtaka la kumuua mumewe usiku wa Desemba 14/15, 2015 katika mtaa wa Kangemi kaunti ya Nairobi.

Maiti ya mumewe ilipatikana na wachimbao mawe katika timbo moja eneo la Lukenya ikiwa imepakiwa ndani ya mfuko.

Mwili wa Ng’ang’a uliokuwa umeoza ulikuwa umefungwa kwa shuka zinazotandikwa kitandani.

Akipitisha hukumu Jaji Mutuku alisema : “Hii mahakama imekupata na hatia ya kumuua mumeo kinyama na kutupa maiti yake ndani ya Timbo katika eneo la Lukenya , kaunti ndogo ya Athi River kaunti ya Machakos.”

Jaji huyo alisema marehemu alirudi nyumbani kutoka kazini na baada ya kula chakula cha jioni wakaenda kulala ndipo mkewe akamuua akiwa uzingizini.

Jaji Mutuku alisema baada ya kumuua mshtakiwa alimkatakata vipande vipande mumewe kisha akaweka ndani ya mfuko maiti yake na kuitupa ndani ya timbo.

Mshtakiwa aliwaeleza wanawe kuwa walivamiwa na majambazi watatu waliotoweka na mumewe. Hata aliwaambia watoto wake na nduguze marehemu alichapwa teke kifuani na wavamizi wao.

Mary aliomba msamaha akisema anaghairi matendo yake.

“Naomba hii mahakama itilie maanani mimi ni kiongozi wa ushirika wa kina mama wakristo wa kanisa Presbyterian (PCEA). Nimesoma na kupata shahada ya diploma katika masuala ya kidini kutoka chuo kikuu cha PCEA Afrika Mashariki,” alisema akijitetea.

Kiongozi wa mashtaka Bi Mercel Ikol aliomba mahakama itilie maanani unyama, Mary muua mumewe.

Jaji Mutuku aliamuru ripoti ya watoto wa marehemu , nduguze marehemu na familia yake iwasilishwe kortini kabla adhabu haijatolewa Oktoba 25, 2018.