Habari Mseto

Mwanamke ashangaza korti kusamehe madume 5 waliombaka

June 7th, 2018 1 min read

Na TITUS OMINDE

MWANAMKE aliyekuwa amedai kubakwa na wanaume watano, Alhamisi alishangaza Mahakama ya Eldoret alipoondoa malalamiko dhidi yao.

Mwanamke huyo aliambia mahakama kwamba kisa hicho kilitokea wakati yeye pamoja na washtakiwa walipokuwa walevi. Alisema aliamua kwa hiari yake mwenyewe kuondoa mashtaka dhidi yao.

Licha ya kuonywa na upande wa mashtaka kuhusu athari ya kuondoa kesi hiyo, mlalamishi alisisitiza kuwa ana haki ya kisheria kuondoa kesi na kuwasamehe washtakiwa.

“Mimi ndiye mlalamishi kwenye kesi hii. Ni kweli kwamba washtakiwa walinibaka kwa pamoja lakini nimeamua kuondoa kesi na kuwasamehe kwa sababu kisa hiki kilitokea wakati sote tulipokuwa walevi,” akasema.

Hakimu alikubali msimamo wake.

Awali mahakama ilikuwa imeambiwa kuwa washtakiwa Kevin Kipkogei, Sammy Kiprono, James Kipritich, James Keino na Isaac Kiptagei kwa pamoja walimbaka mwanamke huyo mnamo Novemba 6, 2012 katika soko la Toiyo-Lok, Eldoret Mashariki.

Washtakiwa hao ambao walikanusha mashtaka walikuwa wameachiliwa kwa bondi ya Sh300,000 kila mmoja.

Kesi hiyo ilikuwa imeahirishwa mara kadhaa kutokana na makosa mbalimbali na wakati mwingine washtakiwa walikuwa hawajiwezi kwa sababu ya ulevi, na hivyo kufanya kesi kuahirishwa mara kwa mara.