Habari Mseto

Mwanamke ashtakiwa kuiba watoto Kisii na kuwauza Nairobi

November 21st, 2020 1 min read

Lydia Nyaboke Charles (mwenye leso ya kijani kibichi) akiwa kortini kwa shtaka la kuiba pacha. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

HUKU polisi wakiendelea kuwatia nguvuni wanaohusika na wizi na ulanguzi wa watoto katika Hospitali ya Mama Lucy, mwanamke mwenye umri wa miaka 33 alishtakiwa kwa wizi wa watoto kutoka kaunti ya Kisii na kuwasafirisha kuwauza Nairobi.

Lydia Nyaboke Charles alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Mutuku akikabiliwa na shtaka la kuwaiba na kuwasafirisha mapacha kutoka soko la Ogembo Kaunti ya Kisii.

Lydia alikanusha mashtaka ya kuwaiba watoto hao pacha waliotambuliwa kwa majina mtoto “A” na mtoto “B”. Alidaiwa aliwalangua watoto hao mnamo Oktoba 14, 2020.

Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka  Bw Anderson Gikunda kwamba Lydia na mwenzake Caroline wakiwa njiaNI kuingia jijini Nairobi watoto hao waliugua ikabidi wawapeleke Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kupokea matibabu.

Bw Gikunda alisema mmoja wa pacha hao aliaga akiwa mle KNH na baada ya kuhojiwa hakuweza kueleza zaidi kuhusu watoto hao ndipo polisi wakaitwa.

Alishikwa akapelekwa kituo cha polisi cha Kilimani na kushtakiwa. Caroline alishtakiwa pia.

Wanawake hao wamezuiliwa hadi Novemba 24 mahakama itakapoamua hatima yao ya dhamana..