Habari Mseto

Mwanamke amuua mumewe kwa kumuuliza sababu ya kuwa mlevi

May 21st, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMKE amemuua mumewe, walipozozana baada ya kuulizwa ni kwa nini alikuwa amerejea nyumbani akiwa mlevi baada ya kutoka kazini.

Majirani walisema kuwa mwanamke huyo wa kijiji cha Kamukunji, Kaunti ya Uasin Gishu waliingia katika ugomvi na bwanake, kwani bwana alitaka kujua kilichomfanya anywe pombe.

“Tuliingilia kati tuliposikia ugomvi na tukaweza kuwatuliza. Tulielewana kuwa walale kisha wasuluhishe ugomvi asubuhi,” majirani wakasema.

Hata hivyo, punde tu majirani hao walipoondoka, wanandoa hao wanasemekana kuendelea na ugomvi, ambao ulisababisha vita na hapo mwanamke huyo aliyekuwa mlevi akamuua mumewe.

Mwili wa marehemu ulipatikana Jumapili asubuhi nyuma ya mlango na mmiliki wa nyumba kwa kuwa walikuwa wakiishi katika ploti ya kukodi, alipoenda kuitisha pesa za nyumba.

Mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya Moi mjini Eldoret, wakati polisi nao walianzisha msako mkali dhidi ya mwanamke huyo ambaye anaripotiwa kutoroka baada ya kutekeleza uovu huo.