Habari Mseto

Mwanamke auguza majeraha, adai mke mwenza kamng'ata

May 10th, 2019 1 min read

Na GAITANO PESSA

MWANAMKE mmoja kutoka kiijiji cha Bujonjori wilayani Bunyala Kaunti ya Busia anauguza majeraha kwenye shavu la kushoto na tumbo na anasema mke mwenza ndiye alimvamia Ijumaa asubuhi na kutekeleza uhalifu huo.

Katika mazungumzo na wanahabari katika zahanati ya Budalang’i anakotibiwa, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 26 na ambaye hatutaji jina lake, amedai kuwa mke mwenza alimkabili asubuhi alipokuwa akilala na kumuuma.

Tukio hilo ambalo limewashangaza wengi lilijiri wakati mme wao alikuwa ameondoka nyumbani kuelekea katika shughuli yake ya kila siku ya kuzoa mchanga; umbali wa kilomita mbili hivi.

“Alipobisha mlango alimweleza mpwa wa mume wangu kuwa alitaka kuzungumza nami nyumbani. Nilijitokeza nikiwa na mwanangu mchanga naye akasisitiza kuwa nimweke pembeni,” alisema mwathiriwa.

Aliongeza kuwa alihisi mambo yalionekana kuchukuwa mkondo mpya mwenzake huyo alipomshurutisha mpwa wa mumewe kuondoka nyumbani; swala ambalo alikatalia mbali huku akimwonya kuwa hana mamlaka ya kuwashurutisha nyumbani mwake.

“Baadaye alinivamia na kuniuma shavuni kabla ya kukwepa na kuniacha nikiwa nahisi maumivu kabla ya kuwahiwa hospitalini.”

Hiki ni kisa cha pili cha uchokozi kutekelezwa na mtekelezaji kosa hilo dhidi ya mwenzake baada ya kile cha kwanza mwaka 2018.

Ni kisa ambacho hakuripoti kwa polisi baada ya “jamaa na marafiki kuingilia kati.”

Msimamizi wa zahanati hiyo Bw Leonard Barasa amethibitisha tukio hilo.

“Tumepokea mgonjwa katika zahanati yetu ambaye aliumwa na mke mwenza shavuni kutokana na mzozo wa kifamilia. Tumemtibu na kumweleza aripoti kwa polisi ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya mshukiwa.”

Tukio hilo la kifamilia linajiri siku chache tu baada ya mwanamume mmoja mkazi wa Wadi ya Bunyala Kaskazini eneo hilo kupata majeraha mabaya baada ya mpenzi wake kumng’ata ulimi wakati mahaba yalipowazidi wakibusiana.