Habari Mseto

Mwanamke avuna Sh3 milioni kwa kuitwa kahaba

June 6th, 2018 1 min read

Na MAUREEN KAKAH 

MWANAMKE aliyetimuliwa kutoka hoteli moja jijini Nairobi kwa kushukiwa kuwa kahaba amefidiwa Sh3 milioni.

Jaji Mbogholi Msagha aliagiza hoteli ya Intercontinental kumlipa Bi Winfred Clarke pesa hizo kwa kumchafulia jina na kuzuiliwa seli kinyume cha sheria miaka 20 iliyopita.

“Vitendo vya hoteli hiyo vilimsababishia mateso na fedheha, amedhihirisha kwamba anastahili fidia na kwa hivyo ninaagiza alipwe Sh2 milioni na hoteli hiyo na Sh1 milioni na Mwanasheria Mkuu,” alisema Jaji Msagha.

Aidha, aliagiza hoteli hiyo na Mwanasheria Mkuu ambao Bi Clarke alikuwa ameshtaki kulipa gharama ya kesi na riba. Kisa hicho kilitendeka Machi 19, 1998 wakati Bi Clarke alienda katika hoteli hiyo kupata kinywaji akiwa na rafiki. Hata hivyo, alisimamishwa na walinzi kwa sababu hakuwa ameandamana na mwanamume.

Alifaulu kuingia hotelini na kuelekea sehemu ya baa ambapo aliagiza chupa mbili za pombe lakini akaambiwa alipe ada ya kumsimamia ambayo hakuelewa ilikuwa ya nini. Alisisitiza kulipa bili yake ya Sh400 pekee.

Aliambia mahakama kwamba wahudumu walikataa kumhudumia na kumtaja kama kahaba mbele ya wateja wengine. Juhudi zake za kueleza kwamba alikuwa mwanamke mwenye heshima na aliyeolewa na Terrence Leonard James Clarke, hazikufua dafu huku walinzi wa hoteli wakimtimua.

Alisema polisi waliitwa kumkamata na kumfungia katika kituo cha polisi cha Central kwa siku mbili.