Habari Mseto

Mwanamke kizimbani kwa kumlazimishia mvulana uroda

January 30th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 23 ameshtakiwa kwa ubakaji kwa kumlisha mvulana wa darasa la nane tunda la ndoa ndani ya seli katika kituo cha polisi.

Binti huyo, Bi Naomi Nechesa Sanya, alifikishwa katika mahakama ya Milimani Nairobi akikabiliwa na shtaka la kumbaka mwanafunzi wa darasa la nane kwa kumlisha mtoto huyo wa miaka 15 tunda lililokatazwa na Mungu.

Nechesa, aliye na mtoto mchanga wa miezi 11 alimlilia hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot amachilie huru akanyonyeshe mwanawe.

“Kama mama naumia kwa vile mtoto wangu hajanyonya tangu nilipokamatwa Januari 27, 2019,” alisema Nechesa.

Akaendelea kurai, “Ni haki ya mtoto chini ya sheria za shirika la umoja wa kimataifa la afya (WHO) kwamba watoto wachanga wanyonyeshwe, wazinyimwe maziwa ya mama hadi wafikie umri wa kuweza kula chakula.”

Mshtakiwa alifahamishwa na mshtakiwa kwamba mtoto wake ameumia tangu Jumapili (Januari 27) na hata “anahisi matiti yake yakiuma kwa vile hayajanyonywa.”

“Nakuomba umwonee mtoto wangu mwenye umri wa miezi 11 huruma kwa kuniachilia kwa dhamana ama uamuru aletwe nitakapozuiliwa nimnyonyeshe,” alisema Nechesa.

Lakini ombi hilo la kuachiliwa kwa dhamana lilipingwa vikali na kiongozi wa mashtaka Bw Kennedy Panyako, aliyeomba mshtakiwa azuiliwe kwa muda wa siku tano zaidi kuchunguzwa kwa kosa la mauaji.

“Naomba mshtakiwa azuiliwe kwa siku tano kusaidia polisi kukamilisha uchunguzi wa kosa la mauaji dhidi yake,” Bw Panyako alimweleza hakimu.

Kiongozi huyo wa mashtaka alieleza mahakama kwamba polisi watampelekea mshtakiwa mtoto wake akamnyonyeshe katika kituo cha Polisi cha Riruta atakapozuiliwa.

Bw Panyako , alimweleza hakimu kuwa itakuwa ni ukandamizaji wa haki za mtoto huyo mchanga kunyimwa mapenzi ya mama na pia kutenganishwa naye kwa siku nyingi.

Bw Panyako pia aliomba korti iamuru kesi hiyo ya ubakaji isikizwe Ijumaa (Februari 1) kwa vile mlalamishi amezuiliwa katika korokoro ya watoto.

“Naomba samanzi zitolewe mlalamishi katika kesi hii ya ubakaji anayezuiliwa katika mji wa kurekebisha tabia ya watoto afikishwe kortini kutoa ushahidi dhidi ya Nechesa,” Bw Panyako alimrai hakimu.

Mahakama iliamuru kesi hiyo isikizwe kesho ndipo polisi waendelee kumchunguza Nechesa kwa kesi ya mauaji.

Lakini mshtakiwa huyo aliishangaza mahakama alipomweleza hakimu, “Ni kweli niliiua. Nataka nisomewe hiyo kesi ya mauaji nikiri nihukumiwe niache kutesekea korokoroni.”

Akitoa uamuzi Bw Cheruiyot aliamuru Polisi wampelekee mshtakiwa mwanawe katika kituo cha polisi cha Riruta kumnyonyesha.

Hakimu alimtaka afisa anayechunguza kesi hiyo atekeleze agizo hilo mara moja.

Nechesa alikana mnamo Januari 27 2019 ndani ya seli katika kituo cha polisi cha Riruta alimbaka mwanafunzi huyo aliyekuwa anazuiliwa kwa kosa la kupatikana na bhangi.

Shtaka badala dhidi ya Nechesa ni kupapasa papasa mwanafunzi huyo sehemu zake nyeti.