Kimataifa

Mwanamke kumnunulia Lindelof chakula cha mchana kwa kumkamata mwizi

August 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BEKI matata wa Manchester United amepongezwa na maafisa wa polisi nchini Uswidi kwa kumkamata mwizi aliyempora ajuza mmoja mjini Vasteras mnamo Agosti 24, 2020.

Kisa hicho kilifanyika kilomita 100 kutoka Jiji Kuu la Uswidi, Stockholm.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mwanamume mwenye umri wa miaka 30 aliyekuwa akiendesha baiskeli alimpkonya ajuza mmoja wa miaka 90 begi lake barabarani.

Inasemekana kwamba Lindelof “alimfuata mshukiwa kwa kasi” kisha akamkwamilia hadi maafisa wa polisi walipofika na kumtia nguvuni mwanamume huyo mwizi.

Katika taarifa yao, polisi nchini Uswidi walisema: “Tunachukuwa fursa hii kumshukuru Lindelof aliyeshuhudia kisa hicho cha wizi na katika busara yake, akajitahidi na kufanya hima kuhakikisha kwamba ajuza aliyeibiwa anapata begi lake.”

Ajuza huyo aliyeibiwa, amejitolea sasa kumnunulia Lindelof, 26, chakula cha mchana kama ishara ya kumshukuru kwa msaada wake.

Mshukiwa aliyekamatwa ameshtakiwa kwa kosa la wizi, uchopozi na matumizi ya dawa za kulevya.

Lindelof aliwajibishwa na Man-United katika jumla ya mechi 35 msimu uliopita na akasaidia kikosi hicho kinachonolewa na kocha Ole Gunnar Solskjaer kutinga nusu-fainali za Kombe la FA na Europa League kisha kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya tatu.