Habari Mseto

Mwanamke motoni kwa kumuua mumewe mlevi

January 16th, 2020 1 min read

Na GEORGE MUNENE

POLISI katika Kaunti ya Kirinyaga wanamzuilia mwanamke ambaye alidaiwa kumuua mumewe mlevi, kisha akaning’iniza mwili wake nyumbani na kudai alijinyonga.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 29, jana alikamatwa na kufungiwa katika kituo cha polisi cha Kianyaga.

Polisi walisema mshukiwa aligombana na mumewe aliyetambuliwa kama Lawrence Kariuki, 36, nyumbani kwao karibu na soko la Kimunye kabla ya wao kupigana.

Hata hivyo, mwanamke alimzidi nguvu Bw Kariuki na kumwangusha.

Hapo ndipo alitia soksi mdomoni mwa mwanamume huyo na kumnyonga hadi akafa.

Baada ya muda, mwanamke huyo alitoa habari kwa polisi kwamba mumewe alijitia kitanzi kufuatia ugomvi wa kinyumbani.

Mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Kirinyaga Mashariki, Antony Wanjuu alisema maafisa wake waliingiwa na shaka walipofika eneo la tukio kufanya uchunguzi na kupata soksi katika mdomo wa mwendazake.

“Hiyo ndio maana tuliamua kwamba maiti hiyo ifanyiwe upasuaji. Na matokeo yamefichua kwamba hakujitia kitanzi bali aliuawa,” akasema.

Bw Wanjuu alisema mwanamke huyo atafikishwa mahakamani hivi karibuni.

“Mshikiwa ametenda kosa mbaya zaidi na sharti akabiliwe na mkono wa sharia,” Bw Wanjuu akasema.

Kabla ya kifo chake, Bw Kariuki alikuwa anafanyakazi ya kushona viatu katika soko la Kimunye.

Wakazi waliohojiwa walisema kwamba mwanamume huyo amekuwa akigombana na mkewe kila anapolewa.