Makala

MWANAMKE MWELEDI: Alijitolea kuwapa maskini mikopo nafuu

April 3rd, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

Baada ya kudumu katika sekta ya ujenzi wa nyumba, Bi Ingrid Munro, msanifu majengo na mtaalamu wa miundo ya miji kutoka Uswidi, alistaafu na kuanzisha hazina ya kutoa mikopo midogo ya Jamii Bora.

Bi Munro aliwahi hudumu katika shirika la UN-Habitat, na pia na serikali ya Uswidi katika kitengo cha utafiti wa makazi kabla ya kuhamia jijini Nairobi, ambapo alihudumu kama mtaalamu wa masuala ya makazi katika shirika la Umoja wa Mataifa na katika harakati hizo kupigania kuwepo kwa makazi ya hadhi kwa maskini.

Shirika la Pan-African inter-governmental Housing na hazina ya African Housing Fund zilipoundwa, Bi Munro alichaguliwa kusimamia mipango hii.

Mpango huu ulinuiwa kukuza miradi mingine katika harakati za kuimarisha makazi kwa watu wenye mapato ya chini. Alisimamia hazina hiyo kwa miaka 11 hadi alipostaafu.

Machi mwaka wa 1999, Bi Munro alitoa mkopo wa US$5 kwa watu 50 waliokuwa wanaishi barabarani ambapo huo ulikuwa mwanzo wa Jamii Bora. Kikundi hicho kiliongezeka kutoka 50 hadi 5000 katika kipindi cha miezi sita pekee, na hapo hazina ya Jamii Bora Trust ikasajiliwa.

Mwaka wa 2010, hazina hii ilinunua benki ya City Finance Trust, na hivyo kuibadilisha na kuwa Jamii Bora Bank.

Bi Munro alitambua kwamba ili kuwepo na mabadiliko ya jumla, basi maskini walihitaji huduma zaidi. Kwa hivyo alianzisha chama cha kuweka akiba na kutoa mikopo ili kusaidia watu wenye mapato ya chini na wanaoishi katika sehemu za mashambani, kuweka akiba na kupa mikopo.

Wakati mmoja Bi Munro aligundua kwamba wanachama wengi walishindwa kulipa mikopo, ambapo baada ya kutembelea wengi wao, alitambua kuwa baadhi yao walikuwa wakiishi maisha ya ufukara, ilhali wengine walikuwa na jamaa wagonjwa, suala lililoathiri uwezo wao wa kulipa mikopo.

Baada ya kushindwa kupata bima ya afya kwa wanachama wake, aliamua kuanzisha bima yake ya afya ambapo wanachama wake na jamaa zao walinufaika. Ni mradi uliopokelewa vyema .

Mbali na mpango wake wa kutoa mikopo na bima ya afya, Jamii Bora ilipanua huduma zake na kuhusisha kutoa huduma ya bima ya majanga (ambapo wanachama wake walioathirika na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008 walilipwa fidia), mafunzo ya wafanyakazi wake (kupitia chuo cha mafunzo ya biashara cha Jamii Bora Business Academy), mpango wa clean-and-sober programme (ili kurekebisha tabia miongoni mwa waraibu wa mihadarati na pombe), na mpango wa kusaidia omba omba mitaani.

Aidha, Jamii Bora ilifungua fursa ya kusaidia wanachama wake kumiliki nyumba, na hivyo kuwapa fursa wakazi wa vitongoji duni kupata makazi ya hadhi.