Makala

MWANAMKE MWELEDI: Alipambana kuhakikisha wakulima wadogo wanaheshimiwa

May 22nd, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KIPAJI chake cha uongozi kimejitokeza kupitia ufanisi wa mashirika mengi chini ya usimamizi wake huku mara nyingi kazi yake ikihusisha mchanganyiko wa utafiti wa kilimo biashara, mauzo, sera, fedha na kilimo uchumi.

Kwa zaidi ya miaka 20 Bi Jane Karuku ameonyesha weledi wake kwa kuongoza mashirika ambayo mara nyingi yalikuwa katika sekta ya kilimo.

Aprili 16, 2012, alijiunga na shirika la Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA) na kuwa msimamizi mkuu wa kwanza wa kike.

Mara nyingi alikuwa mtetezi wa wakulima wadogo ambapo alihakikisha wanapewa heshima waliyostahili.

Kabla ya kujiunga na AGRA, alifanya kazi na shirika la Telkom Kenya, ambapo alikuwa Katibu Mkuu mtendaji kuanzia Julai 2010.

Chini ya uongozi wake katika shirika hili, anatambuliwa kwa kuleta mabadiliko yaliyochangia kuundwa upya kwa shirika hili, na hivyo kulifanya bora na tayari kukabiliana na changamoto mpya za soko.

Awali, alihudumu kama mkurugenzi msimamizi wa Afrika Mashariki katika shirika la Cadbury Schweppes East Africa. Hapa, alikuwa anasimamia shughuli katika nchi 14 barani. Katika kipindi cha hatamu yake hapa, alianzisha mipango kadha wa kadha ya biashara.

Bi Karuku aidha alifanya kazi na mashirika ya Farmer’s Choice na New Kenya Co-operative Creameries (KCC). Pia, ameshikilia nafasi mbali mbali za ushauri katika mashirika mbali mbali ikiwa ni pamoja na Barclays Kenya, Junior Achievement Kenya na United States International University (USIU) jijini Nairobi.

Juni 2013, aliteuliwa na jopo la kilimo, mifumo ya vyakula na lishe bora chini ya serikali ya uingereza, mpango wa kimataifa unaoshauri waundaji sera kuhusu jinsi ya kuwekeza katika kilimo ili kuangamiza njaa na utapia mlo.

Bi Karuku ana shahada ya digrii katika masuala ya sayansi ya vyakula na teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, na shahada ya uzamili katika masuala ya mauzo kutoka Chuo Kikuu cha National University of California nchini Amerika.

Mwaka wa 2015, Bi Karuku alitajwa kama mkurugenzi msimamizi wa Shirika la Kenya Breweries Limited, ambapo pia alithibitisha uwezo wake hapa. Ari yake ni kustawisha bara la Afrika.