Makala

MWANAMKE MWELEDI: Alithubutu kuasi tamaduni za kwao

September 14th, 2019 3 min read

Na KEYB

LICHA ya kutengwa na jamii yake kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya mojawapo ya tamaduni kuu, hakulegeza kamba katika vita vyake dhidi ya ndoa za mapema.

Hii ni shughuli ambayo Priscilla Nangurai aliendesha kwa miaka mingi ili kukabiliana na utamaduni wa kuwaoza wasichana mapema, miongoni mwa jamii ya Wamaasai.

Msukumo huu ulimfanya kuanzisha kituo cha kuokoa wasichana cha AIC Girls Rescue Centre kilichoko katika Kaunti ya Kajiado, kutoa hifadhi kwa watoto wasichana wanaotoroka makwao kuepuka ndoa za mapema. Tangu kuanzishwa kwake, kituo hiki kimesaidia kuokoa zaidi ya wasichana 1,000 kutokana na ndoa za mapema.

Na jitihada hizi zimemfanya kutambuliwa katika majukwaa kadha wa kadha ambapo yeye ni mshindi mara mbili wa tuzo ya The Order of the Grand Warrior (OGW). Pia, mwaka wa 2002 alitawazwa mshindi wa the Guinness Stout Effort Award.

Mzaliwa huyu wa Kaunti ya Kajiado anasema ari hii ilimjia akiwa na umri mdogo. Alikuwa na miaka sita dadake ambaye wakati huo alikuwa na miaka 16 pekee alipoozwa. Babake ambaye wakati huo alikuwa afisa mlinzi wa misitu, mara nyingi hakuwa nyumbani kutokana na shughuli za kikazi.

Huku mamake akijikakamua kuhakikisha kwamba wanawe wanaenda shuleni, babake naye alikuwa na nia ya kuwaoza wanawe.

Anakumbuka jinsi wakati mmoja akiwa katika darasa la sita alikutana na dadake akilia.

“Wakati huo alikuwa katika kidato cha pili katika shule ya upili ya African Girls’ High School- ambayo kwa sasa inafahamika kama Alliance Girls High School, ambapo baba alimzuia kwenda shuleni na kumlazimu kuolewa,” aeleza.

Lakini Bi Nangurai, alibahatika kwani shemeji yake alithamini elimu ya wasichana. Alimsaidia kuhamia katika shule ya msingi ya Ilbissil, ambapo baadaye alifuzu kujiunga na shule ya upili ya Alliance Girls High School.

“Shemeji yangu alinisaidia kupata ufadhili wa masomo ya upili. Kaka zangu wawili ambao wakati huo walikuwa wanafanya kazi, pia walinisaidia wa kuninunulia vitabu na kugharimia mahitaji mengine ya masomo,” aeleza.

Lakini akiwa katika kidato cha tatu nusura ndoto yake ya kukamilisha elimu ifikie kikomo. “Babangu aliniambia kwamba nilipaswa kurejea nyumbani kwani alikuwa amenitafutia mume. Hata hivyo dadangu pamoja na mwalimu mkuu walipigana vikali kuhakikisha kwamba nasalia shuleni. Nakumbuka likizo moja nilikaa nyumbani kwa mwalimu huyo, Bi Okumu,” akumbuka.

Baadaye alijiunga na chuo cha Kenyatta College ambacho kwa sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Kenyatta, mwaka wa 1966 na kupokea mafunzo ya ualimu. Baada ya kukamilisha mafunzo hayo 1968, Bi Nangurai, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 20, alipelekwa katika shule ya mseto ya upili ya Olkejuado High School.

Changamoto kuu ilikuwa kwamba wanafunzi wengi wa kiume hapa walikuwa wamemzidi umri, na hivyo hawakumheshimu.

“Wakati mwingi walituchokoza na kila tulipowashtaki kwa mwalimu mkuu, walihoji kwamba walikuwa na umri sawa nasi, na hivyo walikuwa na haki ya kucheza nasi,” asema.

Mwaka wa 1982, Kanisa la African Inland Church (AIC) lilimpa fursa ya kuwa mwalimu mkuu katika shule ya msingi ya wasichana ya AIC Girls Boarding Primary School. Alikubaliana na fursa hiyo lakini ilikuwa changamoto kuu kutoka shule ya upili na kujiunga na ya msingi.

Aliposhika usukani, shule hiyo ilikuwa na matokeo mabaya ambapo kati ya shule 80 za msingi katika eneo la Kajiado, taasisi hii ilikuwa nafasi ya 72. Baada ya uchunguzi, waligundua kwamba tatizo kuu lilikuwa mimba zisizotarajiwa na ndoa za mapema.

Mwaka wa 1986 mwito wa kuwaokoa watoto wasichana kutokana na utamaduni huu, ulishika kasi. Hii ilikuwa kupitia kisa fulani ambapo pamoja na maafisa wa serikali eneo hilo walilazimika kumuokoa msichana fulani ambaye alikuwa kwenye hatari ya kuacha masomo kwani jamaa zake tayari walikuwa wamepanga kumuoza.

Ni hatua iliyomfanya kutengwa katika jamii na kusutwa na wengi, huku familia yake ikilazimika kuwekwa chini ya ulinzi mkali kutokana na vitisho kutoka kwa wanavijiji.

Huu ndio ulikuwa mwanzo wa shughuli zake za uokozi. Kufikia mwaka wa 1990, alikuwa anwapa hifadhi wasichana 45.

Serikali pia ilimsaidia kuimarisha juhudi zake ambapo alisajili kikundi cha wanawake wa kujitolea ambao walihusika katika jitihada za kutambua na kuokoa wasichana waliokuwa katika hatari ya kuozwa mapema.

Mwaka wa 1992, warsha ya ustawi wa wanawake iliandaliwa katika eneo la Kajiado, na kupelekea kuundwa kwa kamati za wanawake sita kwa kila kata.

Kamati hizi zilianzisha kampeni za kuwarai wazazi kuwaingiza wanao katika shule za mabweni ili kuimarisha uwezekano wa wasichana kukamilisha masomo. Wakati wa likizo, wangealika wazazi kukaa katika mabweni kwa siku tatu ili kuwahakikishia usalama mabinti zao.

Mwaka wa 1993 chama cha Forum for African Women Educationalists (FAWE) kiliundwa ambapo baadaye kilimsaidia Bi Nangurai kujenga kituo cha AIC Girls Rescue Centre in Kajiado, ambacho kwa sasa kinashughulikia wasichana 60.

Mbali na hayo, pia alianzisha shirika la Humanitarian Efforts for Learning of the Girl-Child in Africa (HELGA), vile vile kituo cha Nanana (Naisula Naserian Nabulu) Rescue Centre mwaka wa 2005 baada ya kustaafu kutoka AIC Girls.

Mwaka wa 1996, chama cha FAWE kilipokuwa kinatuza vituo vya kutoa elimu katika sehemu mbalimbali barani Afrika, kituo cha AIC Girls kilikuwa miongoni mwao. Utambuzi huu uliwapa walimu wa eneo la Kajiado ujasiri wa kutoa mafunzo ya kuimarisha elimu ya watoto wasichana.

Huku akiwa na uzoefu wa miaka katika shughuli za kuwaokoa wasichana kutokana na hatari ya ndoa za mapema, Bi Nangurai anafurahia sana kutoa ushauri nasaha na anataka ujumuishwe kama somo katika mtaala wa mafunzo ya walimu.