Makala

MWANAMKE MWELEDI: Alivalia uhusika wa jaji kikamilifu

August 24th, 2019 3 min read

Na KEYB

KWA zaidi ya miongo mitatu alikuwa mmojawapo wa waigizaji waliotupambia televisheni zetu kupitia kipindi cha Vioja Mahakamani kikipeperushwa kupitia kituo cha runinga cha KBC.

Jina lake ni Lucy Wangui mwigizaji ambaye hadi mwaka wa 2015 aliigiza nafasi ya jaji kwa uthabiti na ujasiri licha ya kwamba hakuwahi kusomea kozi yoyote kuhusu sheria.

Ni suala lililomvunia mashabiki kibao huku wengi wakishindwa kutenganisha nafasi yake kwenye televisheni na uhalisi wa maisha kila walipokutana naye njiani.

Wenzake wanamtambua kutokana na bidii na ukakamavu wake na ndiposa sio ajabu kwamba ametambulika katika majukwaa mbalimbali huku akipokea tuzo tofauti ikiwa ni pamoja na Head of State Commendation mwaka wa 2009.

Mwaka huo huo, aliteuliwa kama muigizaji bora wa mwaka katika vipindi vya televisheni kwenye tuzo za Kalasha Film & Television Awards.

Aidha, amewahi kupokea tuzo ya mwanavichekesho bora katika kipindi cha The Churchill Show.

Penzi lake katika uigizaji lilianza akiwa angali mdogo huku ari yake ikichochewa na mamake ambaye bali na kuwa mfanyabiashara, pia alihusika mara kwa mara na uigizaji huku akishiriki kwenye matangazo ya kibiashara kwenye televisheni.

Kama mwanafunzi wa shule ya msingi ya Saint Brigid na ile ya upili ya Shree Cutchi Gujarati Hindu Union School, Parklands, Nairobi aliendeleza kipaji chake cha uigizaji kwa kushiriki drama.

Hata hivyo, alilazimika kusubiri hadi baada ya kumaliza shule ili kuendeleza ndoto yake kama muigizaji.

Fursa kuu ilijitokeza mwaka wa 1975 akiwa katika chuo cha mafunzo ya juu cha Pansom’s Business College, ambacho wakati huo kilikuwa katika barabara Biashara, ambapo alikuwa akisomea ukarani.

Produsa mmoja wa shirika la habari la (KBC) ambalo wakati huo lilikuwa likitambulika kama Sauti ya Kenya (VOA) alikuwa akisaka waigizaji ili kushiriki katika kipindi kipya kwa jina Jamii ya Mzee Pembe.

Alimfahamisha mamake na akamhimiza kushiriki katika majaribio hayo na kwa bahati nzuri alichaguliwa kushiriki kama mmojawapo wa mabinti zake Mzee Pembe.

Lakini babake alipinga vikali akihisi mwanawe angefanya taaluma nyingine ya heshima. Na ili kumwelekeza katika mkondo aliokuwa akitaka, alimtafutia kazi kama karani katika kampuni ya kuoka mikate ya Elliott’s Kenya Limited ambapo alihudumu kwa miaka miwili.

Lakini moyo wake haukuwa hapo huku wakati huo huo akijihusisha katika shughuli za uigizaji katika shirika la VOK. Hii iliendelea kwa muda, lakini uchovu wa kujihusisha na kazi hizi mbili hatimaye ukamlazimu kuchagua moja.

Alichagua uigizaji ambapo haikuwa rahisi kwani uamuzi wake ulimkasirisha sana babake. Lakini kwa usaidizi wa mamake aliendeleza ndoto yake ya sanaa na hasa uigizaji na uandishi wa muziki. Hata hivyo baadaye aligundua kwamba ilikuwa ghali kurekodi muziki na hivyo akaamua kuigiza tu.

Wakati huu, kipindi cha Vioja Mahakamani kilikuwa tayari kinapeperushwa. Safari yake kwenye kipindi hiki ilianza aliyekuwa akiigiza nafasi ya jaji, marehemu Anne Wanjugu, alipojiunga na shirika fulani la habari la kimataifa.

Kushiriki kwake katika kipindi hiki kulimletea umaarufu sio haba, na katika harakati hizo kubadilisha mtazamo wa babake kuhusu mkondo aliochukua kitaaluma.

Aidha, umahiri huu ulimfungulia milango kwenye vipindi vingine ikiwa ni pamoja na Mzima Duni, Chipukizi, Kivunja Mbavu, Darubini na Vitimbi na hivi majuzi Siri na Kona.

Aidha, alipata fursa ya kushiriki kwenye filamu kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na The Mugumo Tree and The Captain of Nakara (2012), Savage Harvest, Coast for Fire, The Baisikol (1997), Saikati II (1992) na The Flame Trees of Thika (1981).

Lakini ufanisi huu haukuja pasipo changamoto. Tatizo kuu alilokumbana nalo lilikuwa kumakinika na uigizaji huku wenzake wakijihusisha na taaluma zingine zilizodhaniwa kuwa za heshima.

Pia ndoa yake haikusazwa. Mumewe, sawa na babake, hakukubaliana na uamuzi wake wa kuwa mwigizaji, licha ya kwamba walipokutana tayari alikuwa katika tasnia hii. Pamoja walijaliwa binti mmoja kwa jina Khadija Ali.

Kwa Bi Wangui, wakati huo ilikuwa vigumu kusawazisha muda wa famiia yake na ratiba yake kali kama muigizaji suala lililomuudhi mumewe, na hatimaye kusababisha kutalikiana.

Baada ya talaka, alilazimika kuishi kwa kipato kidogo hasa ikizingatiwa kwamba nyakati hizo uigizaji haukuwa na malipo mazuri. Kwa kipindi kimoja kamili wangelipwa kati ya Ksh20 na Ksh60.

Tatizo ligine lilijiri baada ya mabadiliko makali kwenye Vitimbi, ambapo pamoja na waigizaji wengine wa zamani waliondolewa, lakini kutokana na ombi la umma wakarejeshwa.

Changamoto yao kwa sasa asema ni kwamba kizazi cha zamani cha waigizaji kimesahaulika huku waliohusika pakubwa kuunda sekta hii wakipuuzwa. Lakini licha ya changamoto hizi, Bi Wangui ananiuia kuanzisha chuo cha mafunzo ya vichekesho na kukuza vipaji vya uigizaji sio tu humu nchini bali pia katika sehemu zingine barani.