Makala

MWANAMKE MWELEDI: Aliweka historia kuwa Afisa Mkuu katika umri mdogo zaidi

November 9th, 2019 2 min read

Na KEYB

JINA lake linatamba katika uwanja wa biashara na ujasiriamali huku jitihada zake zikitambuliwa sio tu humu nchini bali duniani kote.

Mbali na biashara, Bi Adema Sangale anatambuliwa kwa jitihada zake za kupigania haki za watoto wasichana, kwa kuhakikisha kwamba hawakosi kwenda shuleni kutokana na ukosefu wa visodo.

Aliafikia haya alipoanzisha mradi wa Bottom of the pyramid ambapo alifanya hivyo kwa kuongoza jitihada za kuunganisha washikadau kutoka serikalini, vyombo vya habari na mashirika ya kijamii ili kuondoa ushuru kwa visodo.

Lakini hasa anafahamika kama mfanyabiashara, na mjasiriamali, ambapo mwaka wa 2004 jina lake liliingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa afisa mkuu mtendaji wa kwanza mwenye umri mdogo, kuongoza shirika la kimataifa nchini Kenya. Wakati huo alikuwa na miaka 27 pekee.

Wakati huo huo, alishikilia wadhifa huo katika afisi aliyosimamia akiwa Afrika Kusini ambapo alikuwa msimamizi wa mauzo na mawasiliano katika mataifa yaliyoko Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwa ni pamoja na Angola, Ethiopia, Mozambique, Zambia, Uganda, Tanzania, Namibia, Rwanda na Kenya.

Aidha, amewahi kufanya kazi katika Mpango wa Mazingira wa shirika la Umoja wa Mataifa, World Bicycle Relief, shirika lisilo la kiserikali linalonuia kupunguza viwango vya umaskini katika mataifa yanayostawi.

Kwa sasa Bi Sangale ni msimamizi mshiriki wa kampuni inayotoa ushauri wa kibiashara ya C-Suite Africa, iliyoko jijini Nairobi.

Hasa yeye hutoa ushauri ili kusaidia biashara za humu nchini kubadilika kutoka kusimamiwa na mwanzilishi na kuwa na kitambulisho kipana, na hivyo kueneza shughuli zake katika mataifa tofauti.

Mchango wake katika ulimwengu wa kibiashara umetambuliwa sio tu humu nchini, bali pia kimataifa. Agosti 2013, gazeti la Business Daily Africa lilimtaja miongoni mwa wanawake chini ya umri wa miaka 40, wenye ushawishi mkubwa nchini Kenya.

Aidha, aliteuliwa kuwa kiongozi wa kizazi kipya cha viongozi na African Leadership Network. Pia, amewahi hudumu kama mwenyekiti wa chama cha wanawake wafanyabiashara nchini Kenya, kilichoanzishwa na rais wa zamani wa Ireland, Mary Robinson. Vile vile, yeye ni mwenyekiti wa sasa wa muungano wa wanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Harvard barani Afrika.

Mwaka wa 1997 Bi Sangale alihitimu na shahada ya digrii ya usimamizi wa mfumo wa habari (Management Information Systems), kutoka Chuo Kiku cha United States International University Africa.

Baadaye alipata ufadhili wa kimasomo wa Chevening Scholarship na kwenda kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya usimamizi wa kibiashara katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.

Mwaka wa 2015, alihitimu na shahada ya uzamili ya usimamizi wa masuala ya umma kutoka Chuo Kikuu cha John F. Kennedy School of Government, nchini Amerika.

Alijiunga na shirika la Procter and Gamble kufuatia mpango wa uteuzi wa vyuo vikuu. Wadhifa wake wa kwanza ulikuwa naibu msimamizi wa bidhaa za Pampers na Always nchini Kenya.

Baadaye, mataifa ya Nigeria na Poland yaliongezwa chini ya usimamizi wake. Muda ulivyozidi kusonga, aliendelea kupanda madaraka na baadaye aliteuliwa mkurugenzi msimamizi kanda ya Afrika Mashariki.

Akiwa hapo, alianzisha mradi wa Bottom of the pyramid na kuangazia masaibu yanayowakumba wasichana wanaolazimika kukosa kwenda shuleni wakati wa hedhi eti kwa sababu hawawezi kumudu bei ya visodo.

Dhamira hapa ilikuwa kuangazia masaibu ya wasichana kutoka familia maskini, waliolazimika kukosa kati ya siku 4 na 5 kila mwezi eti kwa sababu hawangeweza kumudu kununua visodo nyakati za hedhi.

Mradi huu ulienea katika mataifa mengine Kusini mwa Jangwa la Sahara, India na hata alishirikishwa kwenye matangazo ya kibiashara ya bidhaa za Always, na baadaye katika gazeti la New York Times nchini Amerika.