Makala

MWANAMKE MWELEDI: Ametamba katika sayansi na ukufunzi

November 23rd, 2019 4 min read

Na KEYB

YEYE ni mmoja wa wanasayansi wa kwanza wa kike hapa Kenya na watetezi wa wanawake katika taaluma ya sayansi nchini.

Aidha, Profesa Mabel Imbuga aliwahi kuwa Naibu chansela wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) na hivyo kuwa mwanamke wa tatu nchini kuwahi kusimamia chuo kikuu.

Tangu ajiunge na Chuo Kikuu cha JKUAT, Prof Imbuga amechangia pakubwa kukua kwa taasisi hiyo. Alianzisha mipango ya masomo ya kujilipia hukua akianzia na kitivo cha sayansi, suala lililopunguza utegemeaji wa ufadhili wa serikali.

“Kufikia katikati ya mwaka wa 2013, mpango huu wa masomo ulichangia asilimia 70 ya mapato ya JKUAT,” asema. Aidha, taasisi hii imeanzisha vyanzo vingine vya kuzalisha mapato ikiwa ni pamoja na ushauri wa malipo kutoka kwa wafanyakazi wa chuo kikuu hicho.

Chini ya uongozi wake, Chuo Kikuu cha JKUAT kilitambuliwa miongoni mwa vyuo vikuu 100 bora barani Afrika.

Aidha, chuo hicho kimemakinika na kuwa taasisi ya viwango vya kimataifa kupitia utafiti na ujasiriamali.

Aidha, chuo kikuu hicho kimeanzisha mipango inayohusika na ajenda ya Kenya ya Ustawi. Hii ni pamoja na shahada ya uchimbaji madini na uhandisi wa usafishaji madini, uhandisi wa baharini na uhandisi wa petroli, vile vile mipango inayohimiza teknolojia na kilimo.

Pia, chuo kikuu cha JKUAT kimeanzisha bustani ya mimea katika kampasi ya Juja, ambapo mimea adimu inakuzwa. Maabara yaliyounganishwa na bustani hiii yanasaidia katika utafiti wa sayansi.

Aidha, kwa ushirikiano na wizara ya viwanda, biashara na mashirika, chuo Kikuu cha JKUAT kimeanzisha Nairobi Industrial and Technology Park, bustani ambayo ni jukwaa la utafiti na ubunifu kupitia mafunzo ya kusaidia kuanzisha viwanda vya kukuza biashara ndogo ndogo.

Mwaka wa 2016, chuo kikuu cha JKUAT pamoja na kampuni ya Nissin Foods Holdings Co. Ltd ya Japan, ziliingia katika mkataba wa kujenga kiwanda kinachounda Nissin Noodles, bidhaa zilizoundiwa soko la Kenya.

Penzi lake katika masuala ya sayansi lilianza akiwa mchanga. Katika mtihani wake wa shule ya upili alipita vyema na kujizolea kiwango cha kwanza yaani Division one, kumaanisha kwamba angejiunga na Chuo Kikuu.

Kinyume na wanafunzi wenzake katika shule ya upili ya wasichana ya Alliance Girls High School waliofanya uamuzi wa kusomea mapishi na ushonaji, Prof Imbuga aliamua kujitosa katika hisabati, biolojia, kemia na fizikia.

Anawatambua wazazi wake kwa kuchangia pakubwa ufanisi wake kielimu. “Mamangu na babangu walitaka sana kuwapa wanao elimu nzuri,” asema Prof Imbuga.

Alianza masomo katika shule ya msingi ya wasichana ya Bunyore. Baada ya kupita mtihani wa CPE, alijiunga na shule ya upili ya wasichana ya Alliance Girls High School ambapo alisoma hadi kidato cha sita.

Baadaye alijiunga naa Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alisomea shahada yake ya kwanza, ya uzamili na uzamifu katika Biokemia. “Mimi ni mmoja wa wanafunzi wachache wa zamani wa Chuo Kikuu cha Nairobi ambao wamesomea shahada zao tatu kwenye paa moja,” asema.

Ni kutokana na kujihusisha kwake katika masuala ya sayansi ndipo alijitosa kwenye akademia. Alianza safari yake katika Chuo Kikuu cha Nairobi, huku akipanda katika viwango tofauti, kuanzia mhitimu msaidizi, hadi mkufunzi mshiriki kisha mhadhiri.

Baada ya kuhudumu kama mhadhiri, alipumzika kutoka akademia na kujihusisha na utafiti.

“Nilichukua likizo kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na kujiuga na Kituo cha kimataifa kinachohusika na maumbile ya wadudu (ICIPE).”

Alihudumu hapa kwa miaka mitano ambapo alisomea kozi zingine za baada ya shahada ya uzamifu kisha akawa mwanasayansi wa utafiti. Baadaye alirejea katika Chuo Kikuu cha Nairobi kama mhadhiri mkuu.

Mwaka wa 1997, Prof Imbuga alipata fursa ya kuwa profesa mshiriki wa Chuo Kikuu cha (JKUAT).“Nilipowasili, chuo kikuu cha JKUAT kilikuwa tu kimeanzisha masomo ya bayokemia, kwa hivyo nilikuja kuanzisha idara hiyo.”

Alikuwa mwenyekiti wa idara ya bayokemia, na katika kipindi cha miaka miwili alichaguliwa kama mkuu wa Kitivo cha Sayansi. Kipindi chake cha kwanza kwenye wadhifa huo kilipofikia kikomo, aliingia kenye kipindi cha pili bila pingamizi.

Baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili, Prof Imbuga alichaguliwa kama mkurugenzi wa Taasisi ya dawa za tropiki na maradhi yanayoambukizana. Taasisi hiyo baadaye ilibadilishwa jina na kuwa chuo cha sayansi ya afya (College of Health Sciences). “Ni wakati huu ambapo chuo kikuu cha JKUAT kilitenga nafasi ya Naibu Makamu wa Chansela anayehusika na masuala ya kielimu (DVC AA),” asema.

Prof Imbuga aliteuliwa kama DVC AA mwaka wa 2005 ambapo alishikilia nafasi hii kwa miaka mitatu. Safari yake Prof Imbuga kuelekea juu haikuishia hapo. Mwaka wa 2008 nafasi ya naibu chansela wa chuo kikuu cha JKUAT ilibakia wazi.

Lakini haikuwa rahisi ambapo ilimbidi kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya usimamizi wa biashara katika taasisi ya usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI).

Kama mwanamke anayejaribu kufanikiwa katika taaluma inayotawaliwa na wanaume, Prof Imbuga anasema, “Lazima ujipigane ili kupata unachostahili.”

Kwa mfano akihudumu kama DVC AA, alikumbana na changamoto ya kupata faida zingine zilizoambatana na cheo kama vile kuongezwa mshahara. Lakini hakufa moyo ambapo ushauri wake ni kwamba “Changamoto zitakuwepo kila wakati, lakini lazima usimame kidete, kumakinika na kudumisha malengo yako.”

Mbali na ufanisi wake, mwito wake mkubwa umekuwa kupigania uwakilishi wanawake katika taaluma ya kisayansi. Ni ujuzi wake katika taaluma hii iliyotawaliwa na wanaume iliyomsukuma pamoja na kikundi cha wanawake wengine walioshamiri katika masuala ya sayansi kuanzisha African Women in Science and Engineering (AWSE).

Majukumu makuu ya shirika hili yamekuwa kuhimiza, kuwapa nguvu na kuwanasihi wasichana ili waweze kusomea kozi za kisayansi na uhandisi chuoni.

Kama Naibu chansela, utetezi wa kijinsia umepata kipaumbele. “Tunatia bidii kuhakikisha kwamba wanawake wanaunda asilimia 30 ya wafanyakazi wetu na wanafunzi chuoni.” Kufikia mwaka wa 2013, idadi ya wanafunzi wa kike waliojiunga na chuo kikuu hicho iliongezeka kwa asilimia 17.

Prof Imbuga, ambaye alihudumu kama Naibu Chansela hadi Agosti 2018, anataja mbinu ya uongozi wake kama ya utumishi.

Kuhusu kusawazisha maisha binafsi na kazi anasema kwamba unahitaji usaidizi wa familia yako ili kutimiza ndoto zako.

Taaluma yake ilivyozidi kuimarika, alibahatika kupata usaidizi wa mumewe – marehemu Prof Francis Imbuga, ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na watoto wao.

“Kuna nyakati ambapo angewashughulikia watoto huku nikiwa kazini ambapo angenisubiri hadi niwasili kabla ya kwenda kukutana na marafiki zake. Ni usaidizi wake ulioniwezesha kufanikiwa nyumbani na kazini.”

Kuipa familia yako muda pia ni muhimu. Ana majukumu mengi, lakini anasisitiza kwamba amekuwa akiipa familia yake kipaumbele.

“Nimekuwa nikijitahidi kuwa mke na mama mwema na naamini kwamba nimeweza kufanikiwa katika haya. Usawazishaji wa familia na kazi unahitaji mtu kuwa makini na awe na motisha,” asema.