Makala

MWANAMKE MWELEDI: Bidii imemweka upeoni

March 30th, 2019 3 min read

Na KENYA YEARBOOK

NI mmojawapo wa majaji wenye tajriba pevu zaidi nchini Kenya.

Joyce Aluoch, ni jaji wa kwanza kutoka Kenya kuhudumu katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), wadhifa aliopata miezi mitatu pekee baada ya kupandishwa madaraka na kuwa jaji wa mahakama ya rufaa.

Sio hayo tu! Machi 2015, alikuwa jaji wa kwanza Mwafrika kuteuliwa kama Naibu wa Rais wa mahakama ya ICC ambapo alihitajika kuhudumu katika kipindi cha miaka mitatu.

Jaji Aluoch, ana shahada ya Sheria kutoka Chuo kikuu cha Nairobi na stashahada katika masuala ya sheria kutoka chuo cha Kenya School of Law.

Ajabu ni kwamba, hakuwahi kudhania kwamba wakati mmoja angekuwa wakili.

Baada ya kufanya vyema katika masomo ya shule ya upili alijua kwamba alitaka kuwa mhudumu wa kijamii, wakati huo akifanya kazi katika idara ya uhamiaji.

Babake alikuwa na mawazo tofauti. Siku moja aliandamana naye kazini, na kujipata katika chuo cha mafunzo cha sheria cha Kenya School of Law, ambapo walikutana na mkuu wa chuo hicho.

Ziara hiyo ilithibitisha safari yake katika Uanasheria ambapo baadaye alihitimu kama wakili kutoka chuo kikuu cha Nairobi na kujiunga na idara ya sheria kama Hakimu wa Wilaya pindi baada ya kukamilisha masomo yake.

Alipoanza safari yake katika sheria, alikuwa na ari ya kuendelea kujiimarisha na kupanda ngazi, hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo, idadi ya wanawake katika idara hii ilikuwa ndogo.

Kwa hivyo alijizatiti kuhakikisha kwamba idadi ya wanawake inaongezeka kwa kuendesha mipango ya unasihi kuandaa mawakili wa kike kuwazia kuwa mahakimu na majaji.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwani shughuli ya kusaidia wanawake wanaohudumu katika idara ya sheria kupanda madaraka ilijikokota mno.

“Sio kwamba wanawake hawakuwa wanatia bidii. Tulikuwa tunajitahidi sawa na wanaume, bali na kuwa akina mama na wake. Sikuelewa kwa nini jitihada zetu zilichukua muda mrefu kutambuliwa,” asema.

Licha ya changamoto hizi, Jaji Aluoch aliendelea kupanda madaraka. Alikuwa mwanamke wa pili kuteuliwa kama Jaji wa Mahakama Kuu baada ya mwenzake, Effie Owuor.

Anakumbuka jinsi kama wanawake wawili pekee katika idara ya mahakama, hawakuwa wanapokea marupurupu ya nyumba eti kwa sababu walikuwa wameolewa.

Siku moja wawili hawa walimtembelea Rais katika Ikulu jijini Nairobi na kuangazia matatizo ya wanawake katika utumishi wa umma.

Huenda usawa ambao wanawake katika utumishi wa umma wanashuhudia kwa sasa ni kutokana na matunda ya ujasiri wa majaji hawa.

Changamoto ni zipi?

Ni safari ambayo imekuwa na pandashuka zake.

Aliolewa na kumpata mwanawe wa kwanza akiwa angali mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Nairobi. Anakumbuka jinsi alivyotatizika kusawazisha majukumu ya mama, mwanafunzi na baadaye jaji.

“Nakumbuka wanangu walipokuwa bado wananyonya, ilinibidi kuwa nyumbani wakati wa asubuhi na kuandaa vikao vya mahakama adhuhuri. Hii kidogo ilinirudisha nyuma,” aeleza.

Lakini pia anasisitiza kuwa mama na afisa wa mahakama kulimpa msukumo wa kujizatiti katika taaluma yake.
Baada ya kuteuliwa kama hakimu wa wilaya, Jaji Aluoch alipanda hadi viwango vya Jaji wa Mahakama kuu, nafasi aliyoishikilia kwa miaka 20.

Alikuwa mwenyekiti wa kwanza katika Kamati ya wataalamu Waafrika kuhusu haki na maslahi ya watoto, na naibu mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watoto kati ya 2003 na 2009.

Hii ni kando na kuhudumu katika jopo dhidi ya uhalifu wa dhuluma za kimapenzi, suala lililopelekea kuundwa kwa Sheria ya Dhuluma ya Kimapenzi Mwaka wa 2006.

Jaji Aluoch anataja uteuzi wake kama Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kama ufanisi wake mkubwa.

“Nilishinda kwa kura 100 kutoka mataifa 108. Wakati huo nilikuwa nafanya shahada yangu ya uzamifu na nilikuwa nashughulikia masuala ya Mahakama ya Rufaa, kumaanisha kwamba sikuwa na muda wa kufanya kampeni. Ni Mungu aliyenisaidia,” asema.

Jaji Aluoch alipata shahada yake ya uzamifu katika masuala ya kimataifa kutoka kwa Chuo Kikuu cha Tufts nchini Amerika. Mwaka wa 2015, chuo hicho kilimpa tuzo ya heshima kama mwanafunzi wa zamani na kama utambuzi wa huduma yake kuu katika jamii.

Ufanisi huu haujamzuia kuzidi kuhudumia jamii ambapo alipohamia jijini Hague, alijiunga na chama cha Rotary Club na kuhudumu kama mwenyekiti wa huduma za kijamii.

Mbali na hayo, anazidi kunasihi wasichana kama mbinu ya kujitolea kuhudumia jamii nchini Kenya na Uholanzi.