Makala

MWANAMKE MWELEDI: Mwanamitindo anayekabili funza

February 1st, 2020 3 min read

Na KEYB

YEYE ni mmojawapo wa wanamitindo wa humu nchini ambao umaarufu wao umeendelea hata baada ya kustaafu kutoka ulingo wa uanamitindo.

Cecilia Murugi Mwangi ndilo jina lake, mwanamitindo aliyejitosa rasmi katika uga wa urembo alipotwaa taji la Miss World Kenya mwaka wa 2005 na kuiwakilisha Kenya katika shindano la Miss World, lililoandaliwa nchini China mwaka huo.

Aidha, nyota yake iling’aa mara nyingine mwaka wa 2007 alipoteuliwa mjumbe wa kampeni dhidi ya funza kwa ufadhili wa shirika la Ahadi Trust Kenya.

Ari katika uanamitindo ilianza akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya upili ya wasichana ya State House Girls’ ambapo alishindania taji la Miss State House Girls’ na kumaliza wa tatu. Mwaka uliofuata alishiriki tena na kushinda taji hilo kabla ya kulitwaa tena mwaka uliofuatia.

Baada ya kukamilisha mtihani wa kitaifa wa KCSE mwaka wa 2002, aliahirisha ndoto yake ya uanamitindo, lakini akaamua kuifufua tena baada ya rafiki yake kumshawishi kushiriki katika shughuli fulani ya kupigwa picha. Ni baada ya hapa alijitosa vilivyo katika uanamitindo na mwaka wa 2005 akashinda taji la Miss World Kenya katika jaribio lake la pili.

Mwaka wa 2007, Bi Mwangi alikuwa miongoni mwa kikundi cha watu maarufu nchini Kenya walioalikwa katika warsha iliyoandaliwa na shirika la Ahadi Trust Kenya.

Lengo kuu la shirika hili lilikuwa kukabiliana na tatizo la funza kote nchini, ambapo alikubali mwito huo na hata kutangazwa kama mjumbe wa kampeni dhidi ya funza. Ni kazi ambayo anaendelea kuifanya katika harakati za kuimarisha maisha ya maelfu ya watu katika sehemu za mashambani, ambao hawangeweza kuendelea na shughuli zao za kawaida kutokana na tatizo la funza.

Huku akihudumu na shirika la Ahadi Trust, mwanamitindo huyu ameweza kufungua vituo kadha wa kadha vya kusaidia watu wanaoathirika na tatizo la funza katika sehemu mbalimbali nchini.

Aidha, kampeni hizi zimehusisha mapambano dhidi ya funza kupitia ushonaji vikapu, ufugaji nyuki na shughuli za ujasiriamali ili kusaidia familia husika kujitafutia riziki.

Bi Mwangi pia anafanya kazi pamoja na vijana wanaoishi katika vitongoji duni kupitia shughuli za uhisani ambapo ndoto yake pia ni kuundia wasichana nafasi za ajira.

Alianzisha shindano la urembo kwa jina Miss Mukuru Crown katika Mukuru Kayaba, mojawapo ya vitongoji duni ambapo anahudumu. Baada ya kutambua kwamba wasichana wengi wanaoishi katika vitongoji duni walikumbwa na tatizo la kujithamini, alijitolea kuwanasihi katika harakati ya kubadilisha mawazo yao ili wajiamini.

Taasisi zingine ambazo zimenufaika na miradi ya Bi Mwangi ni pamoja na: Shangilia Mtoto wa Africa, Machakos Community School na Wema Centre.

Kutokana na mchango wake kama mjumbe wa kampeni ya kupambana na tatizo la funza, Bi Mwangi alishinda tuzo ya Young Achievers Award, iliyodhaminiwa na Muungano wa wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mwaka wa 2009, shirika la Ahadi Trust Kenya lilituzwa taji la Leadership & Management Award in Global Health, linalodhaminiwa na shirika la Amerika la ustawi wa kimataifa (USAID). Mwaka huo huo alipokea tuzo ya huduma kutoka Chuo cha sayansi na teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Bi Mwangi aidha alipokea tuzo ya Head of State Commendation kutokana na huduma yake dhidi ya tatizo la funza. Mbali na hayo, kutokana na jitihada zake, Kenya imeorodheshwa ya sita barani Afrika katika harakati za kuafikia Malengo ya milenia (MDGs) 2015 kupitia kampeni dhidi ya funza.

Kando na huduma yake katika shirika la Ahadi Trust, Bi Mwangi pia anafanya kazi na kampuni ya habari na mawasiliano (IT) ya Interstat Limited. Alihitimu na shahada ya digrii ya sayansi katika teknolojia ya kompyuta kutoka chuo cha JKUAT mwaka wa 2008.

Kazi yake hasa inahusisha programu za kompyuta na masuala ya mtandao ambapo anawasihi wasichana kutohofia kujitosa katika tasnia za sayansi kwani hakuna taaluma iliyotengewa tu wanaume au wanawake.

Kwa sasa, Bi Mwangi anaangazia kazi yake katika fani ya habari na mawasiliano, kampeni yake dhidi ya funza, vile vile kumlea bintiye. Anazidi kuwasihi watu wengine kuungana naye katika kampeni yake dhidi ya tatizo la funza.