Makala

MWANAMKE MWELEDI: Mwanasayansi mtajika nchini

January 18th, 2020 3 min read

Na KEYB

YEYE ni mmoja wa wanawake wa kwanza kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi.

Lakini mbali na kustawi katika elimu, alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba suala la hakimiliki linatiliwa maanani nchini Kenya.

Jina lake ni Profesa Norah Olembo, mkurugenzi mtendaji wa the African Biotechnology Stakeholders Forum (ABSF). Kutokana na kuhitimu kwake katika nyanja mbalimbali za kielimu, Prof Olembo anafahamika kama mmojawapo wa wanawake wataalamu wa kwanza wa kike kuwika katika taaluma inayotawaliwa na wanaume.

Hata hivyo, japo alifurahishwa na masuala ya sayansi, mwanzoni safari yake katika nyanja ya sayansi haikuwa mteremko. Prof Olembo alikuwa katika shule ya upili wakati ambapo Baolojia na Hisabati zilikuwa somo peke za kisayansi zilizofanywa na wanafunzi wa kike.

Mwaka wa 1960 alipita mtihani wake wa kidato cha nne, lakini wakati huo bado hakuwa amewahi kusikia kuhusu Fizikia na Kemia. Lakini licha ya hayo, aliamua kufuata ndoto yake katika masuala ya sayansi alipoondoka nchini kwenda katika chuo cha Mount School, Yorkshire nchini Uingereza, kwa kidato cha tano na cha sita.

Ni hapa alitambua upana wa sayansi ambapo alipata hati ya Kemia, Baolojia na Fizikia.

Prof Olembo alirejea nchini Kenya na kuwa mmojawapo wa wanawake wa kwanza kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, ambapo alisomea shahada ya Sayansi katika Kemia, Zuolojia na Botania. Mwaka wa 1972 alihitimu na shahada ya uzamili ya Sayansi katika Zuolojia kutoka taasisi hiyo hiyo.

Aidha, ana shahada ya juu baada ya udaktari katika Baolojia ya Molekuli (Molecular Biology) kutoka Chuo Kikuu cha London, vile vile shahada ya uzamifu katika Biochemistry kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Prof Olembo pia ana hati za kitaaluma ikiwa ni pamoja na Insect Endocrinology kutoka Kituo cha Kimataifa cha Fiziolojia ya Wadudu na Ikolojia (ICIPE) nchini Kenya. Aidha ana hati ya mipango ya kimkakati kutoka Mashirika ya kujitolea kutoa usaidizi wa kiustawi nchini Kenya (VADA), na ile ya Recombinant DNA Techniques kutoka taasisi ya Courtauld Institute of Biochemistry nchini Uingereza.

Kama mmoja wa wanawake wa kwanza kupokea shahada ya uzamifu nchini, Profesa Olembo amehudumu katika nyadhifa mbalimbali kama mwanasayansi, na hivyo kupokea uzoefu mwingi.

Alihudumu kama profesa mshiriki wa Biokemia katika Chuo Kikuu cha Nairobi, na baadaye aliteuliwa kama Mwenyekiti wa Idara ya Biokemia katika taasisi hiyo hiyo.

Mbali na hayo, pia alihudumu kama Mkurugenzi Msimamizi wa Kenya Industrial Property Organisation (KIPO) kati ya mwaka wa 1992 hadi 2002. Taasisi hiyo ilipobadilishwa jina na kuwa Kenya Industrial Property Institute (KIPI), alihudumu kama mkurugenzi kwa mwaka mmoja zaidi.

Kabla ya hapo, Prof Olembo alihudumu kama mshauri wa mashirika mbalimbali kama vile shirika la Chakula na Kilimo (Food and Agricultural Organisation), Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP), Huduma ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo (International Service for National Agricultural Research), Kituo cha kimataifa cha utafiti wa maeneo kame (International Centre for Research in Semi-Arid Tropics) na Kituo cha kimataifa cha utafiti wa mahindi (International Centre for Maize Research).

Amechapisha zaidi ya kumbukumbu 30, muhtasari na taarifa za utafiti katika majarida mbalimbali ya kisayansi kimataifa.

Prof Olembo ni mwanachama wa zaidi ya mashirika 30 ya kitaalamu ikiwa ni pamoja Kamati ya sera za rasilimali za kijenetiki katika Taasisi ya kimataifa ya rasilimali za jeni za mimea (IPGRI), Tume ya Elimu ya Kibaolojia (CBE) ya Muungano wa kimataifa wa wafadhili wa taasisi ya sheria ya umma (International Union Trustee of the Public Law Institute), na Muungano wa wanawake katika taaluma ya Biokemia (International Association for Women Biochemists).

Kama utambuzi kwa mchango wake katika sayansi, Prof Olembo ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya wasichana ya Butere, amepokea tuzo mbili kutoka kwa rais: the Order of the Moran of the Burning Spear (MBS) na Order of the Grand Warrior of Kenya (OGW).

Anaamini kwamba kupitia bioteknolojia, Kenya yaweza kupata njia ya kuzuia uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mbinu za kilimo zilizopo.