Makala

MWANAMKE MWELEDI: Nembo ya uthabiti na ukakamavu katika uanahabari

February 29th, 2020 2 min read

Na KEYB

NI nadra kwa orodha ya wanahabari waliotamba na kuheshimika nchini kuundwa pasipo jina lake kushirikishwa.

Jina lake ni Bi Kathleen Openda Mvati, mtangazaji aliyejiundia jina kama mojawapo ya wanahabari wa kike waliojiundia sifa kwa ukakamavu na uthabiti wake kila sauti yake iliposikika na uso wake kujitokeza kwenye televisheni.

Ustadi wake umetambuliwa sio tu hapa nchini bali pia ng’ambo, suala lililodhihirika wavuti wa Eisenhower Fellowships, ulipomtambua kama mwanahabari shupavu na kumteua kama mwanachama wa ufadhili wa masomo wa Eisenhower na Chevening.

Yeye ni mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Uanahabari (Kenya Institute of Mass Communication) baada ya kutawazwa na Rais Uhuru Kenyatta Julai mwaka wa 2018.

Agosti 2010 alitawazwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Tume ya kitaifa ya Ukweli, Haki na Maridhiano (Truth, Justice and Reconciliation Commission of Kenya (TJRC)).

Kabla ya kujiunga na TJRC, Bi Openda alihudumu katika nyanja ya mawasiliano kama mwanahabari na mshauri wa mawasiliano katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.

Alipokuwa akihudumu katika fani ya mawasiliano, Bi Openda alihudumu katika nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Masuala ya Ushirika katika Benki ya Barclays na shirika la habari la Nation Media Group.

Alikuwa mshauri wa mawasiliano katika TJRC kabla ya kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano katika tume hiyo hiyo.

Akifanya kazi kwenye televisheni Bi Openda alitangaza katika vipindi mbali mbali kwenye kituo cha KTN ikiwa ni pamoja na ‘The Breakfast Show’, ‘Third Opinion’ na ‘Enterprise Kenya’.

Aidha, Bi Openda alikuwa msimulizi wa kipindi cha ‘An African Answer, kipindi kilichoonyesha shughuli za upatanisho baada ya ghasia za baada ya uchaguzi. Kipindi hiki hufadhiliwa na Initiative of Change na kurekodiwa nchini Kenya.

Bi Openda pia alikuwa mwanachama wa baraza la ushauri wa vipindi vya habari (BCAB), wadhifa alioshikilia baada ya kuteuliwa na Baraza la vyombo vya habari nchini; Media Council of Kenya.

Alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, vilevile chuo cha uanahabari cha Chuo Kikuu cha Wales, Cardiff nchini Uingereza, chini ya hazina ya Thompson Foundation.