Makala

MWANAMKE MWELEDI: Polisi wa kwanza wa kike nchini aliyevumisha uskauti kwa ari

November 16th, 2019 2 min read

Na KEYB

ALIKUWA mmojawapo wa wanawake wa kwanza wa asili ya Kiafrika kujiunga na kikosi cha polisi.

Aidha, Bi Elizabeth Nyaruai alikuwa mmojawapo wa wanawake wa kwanza nchini kujiunga na chama cha maskauti na hivyo kuwa kigezo na kielelezo cha mabinti wengi humu nchini.

Anakisiwa kuzaliwa mwaka wa 1928. Ari yake ya kuanza kuhudumia jamii ilijitokeza akiwa angali mdogo ambapo akiwa na miaka 10 pekee alijiunga na vuguvugu la maskauti.

Safari yake kama mhudumu wa kulinda usalama ilianza mwaka wa 1951 pindi baada ya kukamilisha masomo ya shule ya upili.

Kabla ya kujiunga na polisi alikuwa ashapata mafunzo ya ualimu katika Shule ya Upili ya Gateiguru, Murang’a, ambapo alikuwa ameagizwa kwenda kufunza shule ya msingi ya Ngorano, eneo la Mathira.

Fursa yake ya kujiunga na kikosi cha polisi ilijitokeza baada ya yeye pamoja na wenzake kuona tangazo la kikosi cha polisi kwenye gazeti ambapo walikuwa wanaandikisha maafisa wa polisi wa kike.

Miezi kadha baada ya kutuma maombi, maafisa watano wa asili ya Kizungu waliwasili shuleni alipokuwa akifunza na kwenda naye tayari kwa mafunzo katika chuo cha mafunzo ya polisi ya Kiganjo.

Lakini mambo hayakuwa mteremko kwa Bi Nyaruai. Kwanza, alipowasili katika chuo cha mafunzo ya polisi cha Kiganjo, kama mojawapo ya wanawake wa kwanza wa Kiafrika kujiunga na kikosi hicho, chuo hicho hakikuwa na kambi ya wanawake.

Alipewa nyumba ya vyumba vitatu vya kulala ambapo ili kumlinda kulikuwa na tangazo kuwaonya makurutu wa kiume kwamba yeyote ambaye angepatikana karibu na nyumba yake basi angefukuzwa.

Lakini muda wake kama afisa wa polisi haukuwa mrefu. Alihudumu katika kikosi cha polisi kwa miaka mitano tu na kuondoka mwaka wa 1956 wakati ambapo vita vya vuguvugu la Mau Mau vilikuwa upeoni huku akishukiwa kujihusisha na kundi hilo ambalo lilikuwa limepigwa marufuku.

Safari ya Bi Nyaruai katika ulingo wa huduma imekuwa ndefu na kusisimua. Lakini licha ya kujihusisha na mambo mengi, alifurahia sana kuhusika kwake katika vuguvugu la maskauti ambapo hata alipata fursa ya kukutana na mwanzilishi wa vuguvugu hili, Lord Baden-Powell.

Aidha, penzi lake kwa vuguvugu hili lilimfanya kutoa ekari mbili za ardhi yake kwa muungano wa maskati nchini miaka 24 iliyopita.