Makala

MWANAMKE MWELEDI: Sanaa inafanya avume ugenini

October 19th, 2019 2 min read

Na KEYB

YEYE ni mmoja wa wanasanaa na wachongaji sanamu wazaliwa wa humu nchini ambao umaarufu wao umevuka mipaka hadi kimataifa.

Kazi zake Wangechi Mutu hujumuisha aina mbalimbali za sanaa ikiwa ni pamoja na kolagi, video, maonyesho, sanamu, na hasa huhusisha dhamira ya kijinsia, asili na ukoloni.

Baadhi ya kazi zake zimekuwa zikihusisha ghasia na dhana potovu kuhusu wanawake weusi katika jamii, huku kitambulisho chake cha sanaa hasa kikiwa chini ya kitengo cha Afrofuturism. Huu ni mchanganyiko wa ubunifu wa kisayansi ili kuonyesha uhalisi wa ubunifu kwa watu wa asili ya Kiafrika.

Ndio sababu kazi zake Bi Wangechi zimezidi kupata umaarufu nchini na mbali. Mwezi Septemba, 2019 aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kazi zake zilipowekwa kwenye kiingilio cha makavazi ya ­Metropolitan Museum of Art, jijini New York.

Tangu mwaka wa 1996 kazi zake zimeonyeshwa katika sehemu tofauti kupitia maonyesho ya vikundi vya wanasanaa, na pia kama mwanasanaa binafsi. Mkusanyiko wa kazi zake umeonyeshwa katika mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Amerika, Ujerumani, Uholanzi, Uingereza na Canada miongoni mwa sehemu zingine.

Baadhi ya makavazi ambayo yameonyesha kazi zake ni pamoja na San Francisco Museum of Modern Art, The Contemporary Austin (Texas), the Miami Art Museum, Tate Modern jijini London, Centre for Fine Arts jijini Brussels, Studio Museum in Harlem jijini New York, Museum Kunstpalast nchini Ujerumani, Centre Georges Pompidou nchini Ufaransa, miongoni mwa sehemu zingine.

Mwaka wa 2014, ubunifu wake ulionyeshwa katika maonyesho ya sanaa kwa jina Nguvu na Nyoka, katika ukumbi wa maonyesho ya sanaa wa Victoria Miro Gallery, jijini London.

Amewahi kushiriki katika maonyesho ya Prospect 1 Biennial eneo la New Orleans na katika maonyesho ya Gwangju Biennale Korea Kusini. Kazi zake zimeshirikishwa katika maonyesho mbalimbali ikiwa ni pamoja na Greater New York katika kituo cha sanaa cha P.S.1 Contemporary Art Center na makavazi ya Museum of Modern Art jijini New York, miongoni mwa zingine.

Aidha, mbali na sanaa, amehusika katika nyanja tofauti ya video. Mwaka wa 2013, video yake ya kwanza ya katuni kwa jina The End of Eating Everything, iliundwa kwa ushirikiano na msanii Santigold kutoka Amerika.

Na katika harakati hizi anajivunia tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na the Richard Leakey Merit Award, Masters of Fine Art Fellowship, utambuzi aliopata kutoka idara ya uchongaji sanaa ya Chuo Kikuu cha Yale nchini Amerika, Jamaica Centre for the Arts Fellowship, Artist in Residence kutoka kwa makavazi ya Studio Museum, eneo la Harlem nchini Amerika, na tuzo ya mwanasanaa wa mwaka kutoka Deutsche Bank.

Isitoshe, kazi zake pia zimeshirikishwa katika katalogi kadha nchini Amerika, Canada, Ulaya na Australia. Pia, tangu mwaka wa 2002 amekuwa mwanasanaa mhadhiri katika hadhara mbalimbali ambapo sanaa zake zimechapishwa.

Bi Mutu alizaliwa jijini Nairobi mwaka wa 1972, ambapo alijiunga na shule ya Loreto Convent Msongari, kisha baadaye akajiunga na chuo cha United World College of the Atlantic, Wales. Alihamia nchini Amerika katika miaka ya tisini na kuendeleza kipaji chake kama mwanasanaa. Kwa sasa anafanya kazi eneo la Brooklyn, New York.