Makala

MWANAMKE MWELEDI: Sasa yuko mbioni kudumisha amani

June 15th, 2019 4 min read

Na KEYB

YEYE ni mmoja wa wanariadha bora wa mbio za masafa marefu kuwahi kupamba uso wa dunia huku jina lake likitambulika sio tu hapa Kenya, bali ulimwenguni kote.

Huyu si mwingine bali ni Tegla Loroupe, mwanariadha, mwanaharakati wa amani na mhisani.

Hasa anafahamika kwa weledi wake katika uga wa riadha; ustadi ambao umemzolea sifa, nishani na tuzo kochokocho ulimwenguni.

Ni mshindi mara tatu wa mbio za dunia za Half-Marathon huku akiandikisha vitabu vya kumbukumbu kwa kuiwakilisha Kenya mara tano kwenye mbio hizo.

Sio hayo tu, Bi Loroupe ni mshindi mara tano wa mbio kuu za marathoni mijini New York, London na Rotterdam.

Aidha, yeye ni mwanamke wa kwanza Mwafrika kushinda mbio za New York Marathon huku akijivunia kushikilia rekodi kadha za dunia, kama vile mbio za kilomita 21 na kilomita 42.

Kando na masuala ya riadha, ni mwanzilishi wa wakfu wa amani wa Tegla Loroupe Peace Foundation unaosuluhisha mizozo ya kikabila kupitia riadha.

Kutokana na jitihada hizi, maisha ya watu zaidi elfu moja yamebadilika ambapo wezi wa mifugo wamesamehewa huku wengine wakibadili mkondo na kuwa wanariadha. Kwa upande mwingine watoto 400 kufikia sasa wameokolewa na kupata hifadhi.

Kutokana na jitihada hizi ametambuliwa katika majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa Balozi wa Umoja wa Mataifa wa Spoti, wadhifa aliopata mwaka wa 2006, na hivyo kusafiri katika misheni za kidiplomasia pamoja na muigizaji maarufu George Clooney kutoka Amerika.

Aidha, mwaka wa 2009, Rais Mwai Kibaki alimtuza shahada ya uzamifu ya heshima kutoka chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro na baadaye kumpokeza tuzo ya Order of the Golden Warrior (OGW).

Pia, alipokea tuzo ya International Olympic Committee Women and Sport kutokana na uhisani wake. Mbali na hayo, Loroupe pia ametambuliwa na The International Sports Press kutokana na jitihada zake za kuleta amani magharibi mwa Kenya, miongoni mwa tuzo zingine.

Kadhalika, yeye ni mwanachama wa Laureus World Sports Academy, chama cha malegendari wa spoti kimataifa wanaotumia ushawishi wao katika michezo kuleta mabadiliko duniani, huku akiwa Mkenya wa pili kuteuliwa hapa baada ya Kipchoge Keino.

Mzaliwa wa jamii ya Kutomwony, Kaunti ya Pokot Magharibi, kama watoto wengine wasichana, Loroupe alikumbana ana kwa ana na ubaguzi kwa misingi ya kijinsia. Kwanza kabisa, jamii yake haikumakinika na elimu ya mtoto msichana.

Ni suala lililojitokeza hata kwa babake ambaye hakuona umuhimu wa kumuelimisha mtoto msichana hasa ikizingatiwa kwamba mapato ya famila yao yalikuwa kidogo. Lakini kizingiti hiki na vingine havikuzima kiu yake kutaka kwenda shule na kuelimika. Kila alipopata nafasi angesoma vitabu vya kakake alipomtembelea nyumbani kwa shangaziye ambapo alikuwa akihudumu kama yaya.

“Nilisisitiza kwamba nilikuwa nataka kwenda shuleni. Sikuwa na sare za shule ila matambara,” akumbuka.

Hata hivyo, licha ya matatizo haya, alipita mtihani wake na huo ukawa mwanzo wa uanaharakati wake wa kuangazia umuhimu wa kumuelimisha mtoto msichana.

Njia-panda

Baada ya kufanya vyema katika mtihani wa shule ya msingi, babake alimruhusu kujiunga na shule ya upili mradi angekubali kutojihusisha na riadha, mchezo uliomtambulisha tokea shule ya msingi.

Lakini kwa usaidizi wa mamake, Loroupe aliendelea kukimbia hata baada ya kujiunga na shule ya upili.

“Aliponipeleka katika shule ya upili, babangu alinitaka nimuahidi kwamba singejihusisha na spoti na hivyo nilipojiiunga na shule ya upili, sikuwa na kasi ya kutaka kujihusisha na shughuli hii,” aeleza.

Lakini tayari alikuwa ashajiundia jina kwenye mbio za mita 5,000 na 10,000. Matokeo mema uwanjani yalimhifadhia nafasi katika taasisi ya sayansi na teknolojia ya Rift Valley, lakini tamaa yake ilikuwa kujiunga na makazi ya watawa wanawake.

“Msukumo wa kujiunga na utawa ulitokana na maisha magumu nyumbani. Mamangu alikuwa mke wa kwanza miongoni mwa wanne na nilikuwa na ndugu 24. Alivumilia mengi na maisha yake hayakuwa rahisi,” asema.

Safari yake katika riadha ilianza rasmi mwaka wa 1990, pindi baada ya kujiunga na chuo cha mafunzo ya juu ambapo alishirikishwa kwenye kikosi cha mbio za kupokezana vijiti (relay) katika mbio za Chiba Ekiden, nchini Japan.

Lakini huu ulikuwa mwanzo wa changamoto huku tatizo kuu likiwa kuwashawishi wateuzi kuhusu uwezo wake hasa kutokana na udogo wake kimaumbile. Ni matukio yaliyomlazimu kutafuta usaidizi nchini Ujerumani ili aweze kushiriki katika mbio zingine.

Alifanikiwa kuingia kwenye mashindano ya mbio za dunia jijini Stuttgart, nchini Ujerumani, mwaka wa 1993, japo hakuwa kambini na timu ya Kenya. Alimaliza wa nne kwenye fainali za mbio za mita elfu 10,000.

Mwaka huo huo alikuwa mwanamke wa kwanza Mkenya kushiriki kwenye mashindano ya mbio za World Half-Marathon Championships, lakini sio katika kikosi cha Kenya, bali kama mwanariadha huru ambapo alijishindia nishani ya shaba licha ya kuanguka kati kati ya mbio hizo.

“Vyombo vya habari viliangazia masaibu yangu ambapo niliwazia hata kubadili uraia. Nilipata amri ya kukutana na Rais Daniel arap Moi katika Ikulu,” asema huku akinukuu kitabu cha Yoshua 1:9 kwenye Biblia, ambacho anasema kilimpa nguvu wakati huo.

Aling’aa katika mbio kadha jijini New York ila umri wake mdogo wa miaka 20 ulimnyima nafasi kujisajili katika New York Marathon mwaka wa 1993.

Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye alirejea jijini humo na kushinda mbio hizo na kuwa mwanamke wa kwanza Mwafrika kutwaa taji hilo, ushindi alioutwaa tena mwaka mmoja baadaye.

Kufikia hapo alikuwa ameonyesha uwezo wake machoni mwa wateuzi ambapo aliwakilisha Kenya na kuishindia nishani za dhahabu kwenye mbio za dunia za World Half-Marathon kati ya mwaka wa 1997 na 1999, huku akitwaa nishani ya shaba katika mashindano ya World Athletics Championships.

Mwaka wa 1998 alivunja rekodi ya mbio jijini Rotterdam, Uholanzi, ufanisi aliourudia tena mwaka mmoja baadaye katika mbio za Berlin Marathon, na kuandikisha rekodi ya kuwa mwanariadha wa kwanza kutoka Afrika kufanya hivyo. Ushindi huu ulifuatiwa na mwingine kwenye mbio za London Marathon (2000) na Lausanne (2002).

Ari yake ya kujihusisha na masuala ya kuleta amani ilichochewa na visa vya mauaji na wizi wa mifugo vilivyokuwa vimekithiri katika jamii yake. Kwa sasa muda wake mwingi anautumia kuhudhuria mikutano na wahisani wa wakfu wake jijini Nairobi na nchini Ujerumani.

.