Makala

MWANAMKE MWELEDI: Sifa kedekede kwa kazi nzuri

August 10th, 2019 2 min read

Na KEYB

KATIKA nyanja ya sheria, jina lake linatambulika huku akiwa mmoja wa majaji mahiri wa kike nchini.

Jaji Grace Mumbi Ngugi amekuwa akihusishwa na baadhi ya kesi za haiba ya juu nchini, huku maamuzi yake thabiti yakimfanya kuwa miongoni mwa majaji jasiri nchini.

Kinachomtofautisha na wenzake ni kwamba licha ya magumu aliyopitia maishani hasa kutokana na hali yake kimaumbile, ameweza kuandikisha jina lake kwenye orodha ya majaji wanaoheshimika sana hapa Kenya

Kupanda cheo kazini kumetokana na baadhi ya maamuzi yake muhimu mahakamani, suala ambalo limemvunia mashabiki, wapenzi vile vile wakosoaji.

Hasa uamuzi wake wa hivi majuzi uliowazima kuingia afisini magavana na watumishi wengine wa umma wanaokabiliwa na kesi za ufisadi.

Maamuzi haya yalikuwa ushindi katika vita dhidi ya ufisadi, suala lililomlimbikizia sifa kutoka pembe tofauti.

Lakini ujasiri wake hauonekani tu mahakamani kwani pia ni mtetezi wa haki za binadamu. Jaji Ngugi ni mwanzilishi mshiriki wa Albinism Foundation of East Africa, wakfu ulioanzishwa mwaka wa 2008 kwa minajili ya kuhakikisha kwamba maslahi ya zeruzeru yanashughulikiwa, na kwamba watu wanaokumbwa na hali hii pia wanakubaliwa katika jamii. Shirika hili pia huhamasisha umma kuhusu dhana potovu zinazohusishwa na uzeruzeru.

Jaji Ngugi ambaye ni mhitimu wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, pia amehusika kama mtafiti wa shirika la kijamii na uongozi Afrika Mashariki la Series on Alternative Research in East Africa Trust (SAREAT).

Pia, aliwahi kuwa mshauri katika wizara ya Uchukuzi na Shirika la Reli nchini katika mpango wa Resettlement Action Plan 2010.

Mbali na hayo, alihusika katika Tume ya Philip Waki kama mshauri wa kisheria, kwa niaba ya FIDA kuhusu wahanga wa dhuluma za kijinsia wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008.

Ni uthabiti na ushujaa huu ambao umemfanya kutambuliwa katika majukwaa kadha wa kadha. Kwa mfano mwaka wa 2013 alipewa tuzo ya mwanasheria wa mwaka na Mahakama ya Kimataifa (ICJ).

Aidha, ni ushujaa huu ambao mwaka wa 2013 ulimfanya kutajwa kama mjumbe wa Brand Kenya.

Kutokana na hali yake ya uzeruzeru, Jaji Ngugi kila mara alijipata kwenye mwangaza alipokuwa na wenzake.

Mara nyingi mwangaza huu haukuwa mzuri hasa kutokana na hali yake.

Hili halikumzuia kutimiza ndoto yake ya kuendelea na masomo na hata kujiunga na chuo kikuu.

Alijitosa kwa mara ya kwanza katika Uanasheria kama wakili wa Mahakama Kuu mwaka wa 1988.

Baadaye alipanda ngazi na kuwa Jaji wa Mahakama Kuu 2011.

Licha ya ratiba yake kali, alipata muda wa kurejea chuoni na kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha London School of Economics and Political Science, nchini Uingereza.

Aprili 2016 Jaji Ngugi alihamishwa katika kitengo cha Katiba na Haki za Kibinadamu katika Mahakama Kuu mjini Kericho na kwa sasa anahudumu kama Jaji Mkuu mjini humo.